Leo jaridani tunamulika kimbunga Melissa huko Karibea, uhamishaji wagonjwa kutoka Gaza kwenda nchi za nje kupata huduma za kigeni na hali tete kwa watoto nchini Sudan. Mwenyeji wako ni Assumpta Massoi.Katibu Mkuu wa Umoja wa MataifaAntonio Guterres ameonesha wasiwasi mkubwa wakati Kimbunga Melissa kikiwa miongoni mwa vimbunga vyenye nguvu zaidi kuwahi kurekodiwa katika Bahari ya Atlantiki kinaendelea kusababisha uharibifu mkubwa katika eneo la Karibea.Kupitia taarifa yake iliyotolewa leo mjini New York Marekani na msemaji wake Katibu Mkuu amesema kimbunga hicho kimeacha athari kubwa nchini Jamaica, Cuba na Bahamas huku mafuriko makubwa yakiripotiwa pia nchini Haiti na Jamhuri ya Dominika.Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa Duniani, WHO, limeongoza uhamishwaji wa kwanza wagonjwa kutoka Gaza tangu awamu mpya ya kusitishwa kwa mapigano. Katika muda wa siku mbili, wagonjwa 41 waliokuwa katika hali mbaya pamoja na familia zao 145 wamehamishwa kutoka eneo la mgogoro, huku maelfu zaidi wakiendelea kusubiri matibabu ya dharura. Flora Nducha na taarifa zaidi.Nchini Sudan hususani katika eneo la El Faher kusinimagharibi mwa nchi, hali ya kibinadamu inazidi kuwa mbaya kila siku, huku ghasia, njaa, na vizuizi vya utoaji misaada vikiendelea kuathiri mamilioni ya watu wakiwemo watoto waliokwama katika maeneo ya vita. Anold Kayanda na taarifa zaidi.