Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina ambayo Bi. Lucy Githinji, mkazi wa jimbo la New Jersey nchini Marekani amezungumza na idhaa hii baada ya matembezi ya hiari kwa ajili ya kuhamasisha jamii kuhusu saratani ya titi, akisema hakika dawa zinafanya kazi.Mratibu wa Umoja wa Mataifa wa Masuala ya Kibinadamu nchini Sudan, Denise Brown amesema ni kweli wamepokea ripoti za mauaji ya baadhi ya wahudumu wa kujitolea huko El Fasher jimboni Darfur wakati huu ambapo mji huo umetwaliwa na wapiganaji wa Vikosi vya Usaidizi wa Haraka, (RSF).Kimbunga Melissa kimepungua nguvu baada ya kutua nchini Jamaica kama kimbunga cha kiwango cha 5, na kuvunja rekodi ya kimbunga chenye nguvu zaidi, kabla ya kuelekea kaskazini mashariki kupita Cuba hadi Bahamas, na kusababisha mafuriko makubwa, uharibifu na kukatika kwa umeme katika maeneo mbalimbali ya Karibea na Amerika ya Kati.Nchini Cameroon, kufuatia mauaji ya raia wakati wa maandamano ya kupinga kutangazwa kwa Paul Biya kuwa mshindi wa kiti cha Urais kwenye uchaguzi uliofanyika Oktoba 12, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu imeeleza wasiwasi wake juu ya ripoti za vifo hivyo.Na katika Katika kujifunza lugha ya Kiswahili hii leo, mtaalam wetu Onni Sigalla, Mhariri mwandamizi wa Baraza la Kiswahili la Taifa nchini Tanzania, BAKITA. Anafafanua maana za neno "SUMIA."Mwenyeji wako ni Assumpta Massoi, karibu!