Hii leo jaridani tunaangazia Siku ya Kimataifa ya Majiji, vifo na majeruhi vilivyotokea katika maandamano yanayohusiana na uchaguzi mkuu uliofanyika nchini Tanzania na uwezeshaji wa wanawake nchini huko huko Tanzania.Dunia leo ikiadhimisha Siku ya Kimataifa ya Majiji, majiji ya kisasa pamoja na kukumbatia teknolojia yametakiwa kuhakikisha yanazingatia zaidi watu ili wengine wasiachwe nyuma au kutengwa na maendeleo hayo.Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Binadamu imeeleza wasiwasi mkubwa kufuatia vifo na majeruhi vilivyotokea katika maandamano yanayohusiana na uchaguzi mkuu uliofanyika nchini Tanzania tarehe 29 mwezi huu wa Oktoba.Mpango wa “Chaguo Langu, Haki Yangu” nchini Tanzania ni jitihada thabiti zinazolenga kuwawezesha wanawake na wasichana kuishi maisha huru dhidi ya ukatili na vitendo hatarishi. Kwa ufadhili wa Serikali ya Finland, Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA) kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania kupitia Shirika la IPS, linafanya mabadiliko halisi katika jamii.Mwenyeji wako ni Assumpta Massoi, karibu!