Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameonesha wasiwasi mkubwa wakati huu Kimbunga Melissa kikiwa miongoni mwa vimbunga vyenye nguvu zaidi kuwahi kurekodiwa katika Bahari ya Atlantiki kinaendelea kusababisha uharibifu mkubwa katika eneo la Karibea.Kupitia taarifa yake iliyotolewa leo mjini New York Marekani na msemaji wake, Katibu Mkuu amesema kimbunga hicho kimeacha madhara makubwa nchini Jamaica, Cuba na Bahamas huku mafuriko makubwa yakiripotiwa pia nchini Haiti na Jamhuri ya Dominika.Taarifa hiyo imemnukuu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwamba “ana wasiwasi mkubwa” na anashikamana na serikali pamoja na wananchi walioathiriwa vibaya na Kimbunga Melissa.”Katibu Mkuu pia “Amewapa pole familia zote za waliopoteza wapendwa wao katika kimbunga hicho na anawatakia majeruhi wote ahueni ya haraka.”Umoja wa Mataifa umeanza kutoa msaada wa dharura, huku timu zake zikiwa tayari mashinani kusaidia kutathmini madhara na kusaidia juhudi za kitaifa. Pia, umetoa dola milioni nne kwa Haiti na vile vile dola milione nne kwa Cuba kutoka Mfuko wake wa Dharura (CERF) ili kusaidia jamii kujiandaa na kupunguza madhara ya kimbunga hicho.Taarifa hiyo imesema Umoja wa Mataifa uko tayari “kutuma wahudumu wa ziada kwa muda mfupi na kuzindua maombi ya misaada ya dharura kukabiliana na mahitaji ya kibinadamu yatakayosababishwa na kimbunga hicho.”Kimbunga Melissa ni miongoni mwa vimbunga vyenye nguvu zaidi kuwahi kuikumba Karibea, na kinatishia maisha ya mamilioni ya watu kutokana na mafuriko, uharibifu na watu kufurushwa katika makazi yao.