Babananiii

Unapochagua Kazi Zingatia


Listen Later

CHAGUA KAZI UNAYOIPENDA:
Jambo la kwanza na lililo muhimu kushinda mengine yote kuhusu kazi ni kuhakikisha kwamba unaipenda kwa dhati na kufurahia kuifanya. Ziko kazi za aina mbalimbali - k.m. kilimo; ufugaji; biashara; kutoa huduma mbalimbali kama vile ualimu; udaktari; ukarani; n.k. Kazi hizo zinaweza kufanywa mahali mbalimbali - k.m. kijijini; mjini; nyumbani; ofisini; kiwandani; n.k. Vile vile kazi hizo zinaweza kufanywa kwa njia mbalimbali - k.m. Kiujamaa; kiushirika; kwa kuajiriwa; kwa kujiajiri mwenyewe peke yako; n.k. Mambo yote haya, pamoja na hadhi ya kazi yenyewe katika jamii unamoishi huenda pia yakaongezea kukufanya upende kazi moja kuliko nyingine.
Kwa vyovyote swali la kwanza la kujiuliza mwenyewe ni hili; *"Kama kazi zote hizo zingeweza kuniletea kipato kilicho sawa, na kama uwezo wa kujipatia kazi zote hizo ungekuwa ni sawa; je, moyoni ningependelea na kufurahia zaidi kufanya kazi zipi?"*
Tayarisha orodha ya kazi zote zile ambazo unazipenda moyoni, ukianzia na kazi zile ambazo unazipenda zaidi kushinda nyingine.
*"Unapotayarisha orodha hii jitahidi sana usiingiwe na mawazo yoyote yanayohusu mshahara au kipato cha aina yoyote."*
CHAGUA KAZI UNAYOIWEZA:
Hatua ya pili katika kufanya uchaguzi wa kazi inayokufaa ni kuchunguza kwa makini orodha yako uliyoitayarisha ya kazi unazozipenda ili uone kwamba ni kazi gani miongoni mwake ambazo utaweza kuzimudu. "Haina maana kufanya kazi usiyoiweza eti kwa kuwa unaipenda.* Kuna mambo mbalimbali ambayo lazima uyatupie macho wakati wa kuamua jambo hili la uwezo wako kuhusu kazi fulani fulani. Kila inapowezekana yafaa uombe ushauri kutoka kwa watu unaowaamini na wanaokufahamu vizuri (k.m. waalimu wako, wazazi, rafiki n.k.) Hawa wataweza kukuambia udhaifu wako na uwezo wako kuhusu kazi unazozipenda.
Baadhi ya mambo muhimu ambayo lazima uyapime mwenyewe au uyaombee ushauri ni haya yafuatayo:-
*1. Maarifa:*
Je, unao ujuzi, au elimu, au kipaji au mazoea, au wepesi wa kujifunza kufanya kazi hiyo unayoipenda?
*2. Afya:*
Je, afya yako itakuruhusu kufanya kazi hiyo bila matatizo yoyote?
*3. Tabia:*
Je, tabia yako inaoana na kazi hiyo? Kwa mfano kama kazi hiyo inahitaji uvumilivu na wewe ni kijana asiye mvumilivu, basi kazi hiyo haikufai ijapokuwa unaipenda.
*Kama wewe ni mtu unayetamani kudokoa dokoa, usilogwe ukachagua kazi ya kutunza fedha, kwani hiyo hatimaye itakupeleka jela.* Vijana wengi waliokimbilia kushika kazi wanazozipenda bila ya kujipima vizuri kiuwezo, wameandamwa na majuto. Ni juu yako uchunguze kwa makini ile orodha yako uliyoitayarisha na kuondoa au kufuta zile kazi ambazo una mashaka kwamba hutazimudu vizuri kielimu, kiafya, kitabia n.k.
*Baada ya kufanya hivyo panga upya kazi zilizosalia katika orodha hiyo ukianzia na kazi zile ambazo una hakika nazo zaidi kwamba utaziweza kuzimudu bila wasiwasi.*
AHSANTENI SANA..... Tutaendelea sehemu nyingine kesho!!! Muwe na usiku mwema!!
...more
View all episodesView all episodes
Download on the App Store

BabananiiiBy Fabian C. Mwakabanje