Karibu kwenye taarifa yetu ya khabari ya leo Ijumaa tarekhe 3 Julai, 2020 kutoka Dawati la Khabari la Oman kwa Kiswahili, Maskat, Oman.
https://covid19.moh.gov.om/#/home (Wizara ya Afya) imetanganza kuwa watu wengine 1,374 walioambukizwa virusi vya Korona wamesajiliwa, na hivyo kuifanya idadi ya waliotambuliwa kuwa na maradhi ya COVID-19 nchini Oman kufikiya 43,929 wakiwemo 193 waliofariki na 26,169 waliokwisha kupona. Wizara hiyo imesema kuwa katika kipindi cha saa 24 zilizopita, watu 5 wamefariki na watu 851 wamepona maambukizo ya virusi vya korona.
Waziri wa Afya, Tabibu, ameungana na uamuzi wa wizara ya ajira wa kuongeza adhabu kwa mashirika ya binafsi ambayo hayafuati masharti yaliyowekwa kwenye kuzuwia kusambaa virusi vya korona nchini Oman. Akizungumza hapo jana kwenye mkutano wa 12 wa Lujna Kuu ya Kupambana na Janga la COVID-19, Tabibu Ahmed Al Saidi alisema kwamba umefika wakati wa wavunjaji wa taratibu hizo kuongezewa adhabu na pia majina yao kutajwa hadharani, akisisitiza kwamba kusambaza virusi vya korona kwa makusudi ni sawa sawa na kutenda kosa la mauaji. Waziri huyo aliuhakikishia umma kwamba bado vituo vya afya nchini Oman viko imara na vinamudu kuikabili hali ya maambukizo juu ya ya kupanda kwa kasi ndani ya kipindi cha majuma sita sasa.
Mkuu wa Ndaki ya Maendeleo ya Oman, https://odb.om (ODB), Daktari Abdul Aziz Al Hinai, amesema kwamba katika kutekeleza maagizo ya Jalatu A'Sultan Haitham bin Tarik yaliyoidhinisha mpango wa mikopo ya dharura isiyo na riba kuwasaidia wafanyabiashara walioumizwa sana na janga la COVID-19, Lujna Kuu imeikabidhi https://odb.om (ODB), mpango huo, ambayo nayo itashirikiana na idara nyengine kuukamilisha. Idara hizo ni Mamlaka ya Mashirika Madogo na ya Kati, maarufu kama Riyada, na Mfuko wa https://www.alraffd.gov.om (Al Raffd). Kwa mujibu wa mkuu huyo wa Ndaki ya Maendeleo ya Oman, miongoni mwa watakaonufaika na mpango huo ni wale ambao wanatumia muda wao wote kusimamia biashara zao kama vile wamiliki wa khuduma ya gari za kuajiri na vyuo vya kufundisha uendeshaji gari, wajasiriamali wa kike, khasa kwenye maduka ya urembo na vipodozi na vituo vya chekechea.
Kwenye khabari za uchumi na biashara, mapato ya Shirika la https://omanlng.co.om/en/Pages/HOME.aspx (Oman LNG) linalomilikiwa yalifikia dola za Kimarekani bilioni 3.485 mwaka jana, 2019 - mwaka ambao ulishuhudia kiwango kikubwa cha usafirishaji mizigo. taarifa ya kila mwaka ya shirika hilo iliyotolewa jana inasema kuwa mapato hayo ni ya chini kidogo ya mwaka uliotangulia, ambapo shirika hilo lilikusanya jumla ya dola bilioni 3.505, juu ya kuwa kodi iliyolipwa na shirika hilo kwa mwaka jana ilikuwa kubwa kwa kiwango cha dola bilioni 1.112 ikilinganishwa na dola bilioni 1.079 mwaka juzi. Waziri wa Mafuta na Gesi na ambaye pia ni mwenyekiti wa Baraza la Wakurugenzi wa https://omanlng.co.om/en/Pages/HOME.aspx (Oman LNG), Daktari Mohammed bin Hamad Al Rumhy, amesema kuwa shirika hilo linavuna mafanikio ya uwekezaji wake kwenye miradi kadhaa.
Kwenye utabiri wa hali ya hewa, http://www.met.gov.om/ (idara inayotabiri hali ya hewa) inasema kutakuwa na mawingu ya hapa na pale katika majimbo ya Dhofar, Al Wusta na Al Sharqiya ya Kusini, ambako pia kuna uwezekano wa kunyesha mvua ndogo ndogo na upepo mkali. Kwa ujumla, Oman nzima itakuwa na anga safi isipokuwa mvua za hapa na pale kwenye Milima ya Al Hajr na maeneo ya jirani kuelekea saa za jioni. Ukungu utakuwepo saa za alfajiri kwenye pwani za Bahari ya Arabuni.
Tunakukumbusha kuwa unaweza kupokea taarifa zetu za khabari kupitia Apple Podcast, Google Podcast, Spotify na vituo vyengine vya Podcasts. Unachotakiwa kufanya ni kupakia Podcasts yoyote kati ya hizo kwenye simu yako ya mkononi na ikisha, kutafuta Oman Kwa Kiswahili na kujisajili kwenye mkondo wetu. Hii ndiyo njia bora kabisa ya kutusikiliza kila siku kwa sababu utapata taarifa moja kwa moja na mapema zaidi kwenye simu yako.
Ukiwa na masuala au fikra maalumu kukhusu matangazo haya ya khabari na utapenda...