Kama wewe ni mtumiaji wa mtandao wa Facebook huenda umewahi kukutana na chapisho linalohusu fursa ya mikopo kutoka kwenye taasisi ya mfanyabiashara bilionea nchini Tanzania Mohamed Dewji Foundation
Sehemu ya chapisho hilo lianasomeka ‘𝐉𝐈𝐏𝐀𝐓𝐈𝐄 𝐌𝐊𝐎𝐏𝐎 𝐊𝐔𝐓𝐎𝐊𝐀 𝐌𝐎𝐇𝐀𝐌𝐄𝐃 𝐃𝐄𝐖𝐉𝐈 𝐅𝐎𝐔𝐍𝐃𝐀𝐓𝐈𝐎𝐍 kwa maelekezo ya kupata vigezo na masharti njoo hwatspp kwa no👉🏿 0748923136’.
Chapisho hilo pamoja na kuhamasisha watu kuomba mikopo wametaja kigezo cha kutoa kwanza kiasi cha hisa ya mkopo unaotaka kupewa kabla ya kupata mkopo wenyewe.
Ufafanuzi zaidi wa taarifa hiyo unaonesha kama unahitaji kukopa Sh100,000 basi utalazimika kutoa kwanza hisa ya Sh22,000 ndipo upewe mkopo huo.
Taarifa hiyo imesambaa katika mtandao wa Facebook kupitia akaunti zenye majina tofauti tofauti toka mwaka 2022 huku ikiwa imeambatanishwa na video fupi inayomnukuu Mohamed Dewji kuwa anatoa mikopo.
Hata hivyo, Habari hiyo haina ukweli wowote kwa kuwa ni habari za uzushi zinazotumiwa na matapeli kuwalaghai wananchi na kujipatia vipato kwa njia zisizo halali.
Nukta Fakti imefanya utafiti ili kubaini ukweli wa akaunti hizo za mtandao wa Facebook na kugundua kuwa akaunti hizo hazina uhusiano wowote na Mohamed Dewji mwenyewe au taasisi yake ya Mohamed Dewji Foundation.
Akaunti sahihi ya Facebook ya mfanyabiashara huyo maarufu nchini ni Mohammed Dewji huku ile ya taasisi yake ni Mo Dewji Foundation na sio Mikopo Tanzania kama inavyojitambulisha akaunti hiyo inayodai kutoa mikopo.
Mohamed Dewji hatoi mikopo
Utafiti zaidi uliofanywa na Nukta Fakti umebaini kuwa, si Mohamed Dewji mwenyewe wala taasisi yake ambayo inajihusisha na utoaji wa mikopo kwa namna yoyote ile.
Kupitia mtandao wa Linkedin Mohamed Dewji amewahi kutoa taarifa kwa umma akifafanua kuwa taasisi yake inajihusisha zaidi kutoa misaada ya kielimu kwa kufadhili masomo, upatikanaji wa maji pamoja na kutatua changamoto katika sekta ya afya.