
Sign up to save your podcasts
Or


Jina MC Gara B ni miungoni mwa majina makubwa sana kwenye ulimwengu wa kazi ambayo mwenzetu huyu amechagua kuifanya. Familia yake, mke na watoto, wazazi wake na wa mkewe pengine, Ndugu jamaa na marafiki na waajiriwa wake wanakula vizuri kwasababu ya kipaji chake Ndugu yetu huyu. Ni mwanaume ambaye akiwa kazini kwake furaha na burudani ambayo huwapa wateja wake ndo inayomfanya azidi kuenda mbali kwenye tasnia hiyo ya ushereheshaji. Again, yeye ni mmoja ya BORA kadhaa ambao wanafanya kazi kama yake.
Mtandao wa kijamii ni kitu kimoja chenye nguvu sana kwenye miaka ya hivi karibuni, kwa ushahidi tulonao tushawaona wengi ‘wakitoboa’ kwasababu ya Instagram au sehemu nyengine. Mitandao iko mingi na kila mmoja na tobo lake la kufikia mjini. Kazi ambayo MC huyu huifanya yeye huenda na team yake kuiweka vizuri kisha ana post kwenye page yake yenye watu karibia MILIONI MOJA NA NUSU. Akizifikisha mjini kazi hizo wengi huvutiwa nazo na ambao wanakua wana shughuli nao bila ya shaka watamtafuta na kutaka kufanya nae kazi. Ubunifu wake ni wa kipekee kutokana na vingi na wengi ambao tumekua tukiwaona kwa miaka mingi sasa. Mtandao wa kijamii umemsaidia na unaendelea kumfanya awe bora zaidi ya jana.
Sasa, shughuli hii anayo ifanya ndo ambayo ilikua ndoto zake? Pengine alikua huku anamuona mtu fulani akiwa anaifanya hii kazi kwa ufanisi na ikamvutia? Ilikuaje mpaka akaingia huko? Kwa kumtizama haraka haraka tu utagundua Ndugu yetu ni MCHESHI, yeye anapenda kucheka na kuongea, ingawa hapo kwenye kuongea nako sio kiviiiile ila ni mtafutaji ambaye AMETIMIA. Story yake alotupa kwenye episode hii inajumuisha yeye kufanya kazi zaidi ya mbili kwenye kipindi flani hivi cha maisha yake ili aweze kuishi vizuri. Ki professional mwenzetu ni MWALIMU, ambaye hiyo kazi aliifanya hasa, na akaijumlisha na kazi ya huduma kwa wateja pale Tigo na wakati huo huo akawa anafanya kazi kwenye kiwanda kimoja hivi huko Pugu Road, hakua na wa kumdekea wala kumsubiria na hustle yake hiyo ndo ambayo anaenda nayo mpaka leo kwenye maisha yake.
Sasa kama Baba na mume kwa mkewe kipenzi ambaye naye alikutana nae sehemu ya kazi yake, Gara B ananijibu kuhusu uaminifu ambao anao kwa mkewe ambaye kwa mujibu wangu kama amekutana nae kwenye mazingira hayo, vipi hujiskia kila mara anapokua kazini mumewe ukichukulia huko ndipo walipo kutana na ndo ambapo wanawake wengi wazuri huwepo? Jibu lake lilikua na kuukonga moyo.
Alituhadhia pia kuhusu wazazi wake na jinsi ambayo ameweza kujitengenezea jina, siku ya kwanza alipopata kimeo cha ku host harusi ya watu ambayo kwa mujibu wake aliibembeleza sana na hakua amepewa nafasi, ila nafasi ilipojileta akanyoosha kwa umbali mrefu mpaka mengine yamebaki story tu. Na hii ndo ilikua simulizi yangu bora kabisa kuhusu kupata nafasi na kuzitumia vyema.
Yangu matumaini utaskiliza na kuangalia kwa makini maana humu anatupa simulizi zote za kutokata tamaa na jinsi ya kuchukua nafasi, ila pia anatuhadithia baadhi ya mitihani ambayo huja na umaarufu pia na jinsi ya kupambana nayo. Mimi nili enjoy na natumai itakua hivyo kwako pia.
Happy Holidays.
Love,
Salama.
Baraka Kizuguto si moja ya majina yajulikanayo miungoni mwa wa Tanzania wengi ambao asilimia kubwa ya wenye simu za mkononi hupendelea zaidi habari za maisha ya watu maarufu na mashuhuri, kutaka kujua wanakula nini, wanaishi wapi, wanalala wapi, wanalala na nani na kadhalika. Na kama wewe ni mmoja wa watu hao na si mpenzi wa mpira basi kumfahamu mgeni wetu wa kwenye kiti chakavu wiki hii itakuwia vigumu. Ila kwa wale watu wa mpira, au wafanyakazi kwenye Vyama vya mpira hapa kwetu na Afrika kwa ujumla au wachezaji au waalimu wa mpira jina na sura yake si ngeni kabisa kwao. Mimi na yeye tulifahamiana hapa mjini miaka kadhaa iliyopita na rafiki yetu mmoja ndo alituunghanisha. Mapenzi yangu kwa mpira wa miguu nayo yalifanya urafiki wetu ukolee zaidi, amekua kiungo kwenye mambo yangu mengi yanayohusiana na kiwanda hiko kwa muda sasa. MSHAURI wangu pia baada ya mimi kupata kibali cha kuweza kuwasisamia wachezaji wa mpira wa miguu duniani. Yeye ni mtu ambaye anawajua wachezaji karibia wote wanaocheza mpira nchi hii na nje, na msaada wake kwangu ni wa kipekee kabisa. Nia na madhumuni ya kusema aje tuongee nae kwenye kipindi chetu ni kwasababu ambazo nimezieleza hapo juu kwenye wasifu wake. Waswahili wanasema ‘kizuri kula na nduguzo’ na kwa msaada na elimu ambayo mimi hupata kutoka kwake nikasema kwanini sasa tusimlete mezani na wengine wakamsikia? Ukichukulia suala la ajira mi kipengele kweli kweli kwenye nchi yetu. Baraka yeye ana ajira ambayo kama tukimsikiliza vizuri basi wengi wanaweza kuchagua njia hiyo na wakapata chochote kitu. Sasa NINI ambacho Baraka hufanya? Kwenye episode hii anatuelezea majukumu yake ya muda mwingi kutoka Shirikisho la Mpira wa miguu Tanzania na Shirikisho la Mpira la Africa. Kukiwa na michezo mbali mbali kama ya nchi na nchi, au klabu kwa klabu yeye ndo huwa msimamizi wa kwanza kwenye michezo hiyo. Safari za kila wikiendi haziishi na kaniambia nidhamu na kujifunza kila siku ndo msingi wake, na je ungependa kujua kikubwa zaidi ambacho ni muhimu kuliko hayo yote? Baraka anasema ni kuweza kuheshimu WAKATI. Hiyo ndo siri ya mafanikio yake, na ndo siri ya yeye kuweza kupata kazi zaidi na zaidi na kuheshimika pia. Kama akiwa kapangiwa mechi ya kusimamia tuseme nchini Angola, labda Kuna mechi kati ya Angola na pengine Madagascar au mechi za klabu kutoka nchi hizo, yeye ndo anakua wakwaza kufika kabla ya team na waamuzi. Kazi yake ni kuhakikisha kila anaye husika na mchezo huo anafanya jambo lake kwa wakati unaotakiwa. Ukaguzi wa hoteli watakazokaa wageni wa mchezo, waamuzi, team, jinsi watakavyoenda uwanjani, mikutano ya waandishi wa habari, ulinzi wa waamuzi wa mchezo huo, kuhusu ball boys, jinsi team zitakavyo ingia uwanjani, kuhakikisha mchezo unaanza kwa wakati na kila kitu kwenda sawa sawa. Jinsi ambavyo unafanya kazi yako vizuri ndo jinsi ambavyo Shirikisho linakuamini na ndo ambavyo CV yako inazidi kukua. Kwahiyo mmoja anawezaje kupata nafasi ya kufanya hayo yote? Yeye aliwezaje mpaka akafika huko? Nini challenge ya hizi kazi? Je kuna ambao Shirikisho linawaandaa kwaajili ya kuzifanya kazi hizo pia? Na wako wangapi ambao wanaliwakilisha Taifa kwenye hiyo kazi? Na je vipi kuhusu malipo yake? Ni kitu ambacho mmoja anaweza kusema ndo anataka kukifanya kama kazi? Misingi yake ikoje? Mtu anatakiwa aanzie wapi hasa? Na ni kitu ambacho anaweza kufanya kwa muda gani mpaka afikie huko ambako yeye yupo sasa? Vipi kuhusu FIFA? Huko yeye ana mpango nako? Ki ukweli yalikua mazungumzo mazuri kwangu na kwake na natumai pia yatakua na uzito flani kwako na kama si kwako ambaye ushajichagulia cha kufanya, basi hata kwa mwengine ambaye unamjua na ana interest na mpira ukamuelekeza juu ya hili. Tafadhali enjoy.
Love,
Salama.
Habibi Masoud Kipanya ni Ally Masoud Nyomwa ambaye ni LEGEND. Kwa mujibu wake alizaliwa huku kakunja ngumi na dhana yake ni kwamba alizaliwa ili awe bondia! Kwa anacho kifanya na ambacho amekua akikifanya tena kwa ufasaha kwa miaka nenda miaka rudi bila ya shaka ni UBONDIA. Hakuna ambaye atabisha juu ya hilo. Amekua akipigania mambo tele na kuyasemea mengi pamoja na kuchekesha na kuelimisha kupitia kalamu yake. Kwa mujibu wake yeye ni mbobevu katika taaluma ya kupuuza na kuchukulia mambo poa kwa kipindi sasa. Lakini pia anaamini yeye ni MTATA. Tukienda mbele na kurudi nyuma, hapo kwenye UTATA hakuna ambaye anaweza kumbishia, hasa kwa wale ambao kalamu yake imewanyoosha kwa kiasi kikubwa.
Mimi na yeye tulikutana kwa mara ya kwanza takriban miaka kumi na tisa iliyopita, wakati huo mimi mbichi hasa na yeye akiwa kashajielewa na chemchem yake ya kipato tayari ilikua inatoa neema. Mimi nilikua ndo kwanza naanza kazi ya kujishikiza pale Times FM kipindi hiko bado ilikua kule Kamata. Masoud alikua analichorea gazeti la Majira ambalo lilikua liko kwenye mwamvuli mmoja na Radio ambayo nami nilikua nimejishikiza baada tu ya kumaliza skuli. Urafiki wetu ulikuja naturally tu maana sote tunapenda kucheka. Kupitia Zuhura Yunus na Binti mwengine wa kuitwa Rahma ndo mimi naye tulifahamiana. Wakati huo yeye alikua na gari kwahiyo lifti za hapa na pale zilikua hazikauki. Pia tulikua tunaitumia gari yake kama sehemu ya ku chill na kuskiliza muziki kwenye parking za Times FM.
Huwezi kukaa kwenye tasnia moja kwa muda mrefu kama wewe si hodari na mwenye kujielewa. Moja ya vitu ambavyo naviusudu kutoka kwake ni uelewa wake wa mambo tele wa tele, IQ yake ni ya juu sana na jinsi ambavyo ana reason ndo huwa anamaliza kabisa, kama binadamu wakati mwengine ni bora kukubaliana kuto kukubaliana na kwakwe yeye wakati mwengine jinsi anavyo wachora baadhi ya matukio na watu huwa haviishii kuzuri lakini hiyo haikuwahi kuwa sababu ya yeye kuacha kufanya ambacho anakifanya na ambacho amekua akikifanya kwa muda sasa. Uelewa wake kwenye mambo ambayo yanaendelea, uwezo wake wa kuona mbali na kuweka sanaa yake hiyo kwenye karatasi kisha kutuachia sisi tung’amue maana yake kwa kweli ni kipaji cha kipekee ya sana. Mmoja anatakiwa akae tu mbali na ku admire akifanyacho na hiko ndo ambacho mimi nimeamua kufanya.
Nilikua nataka anielezee maana halisi ya baadhi ya michoro yake ambayo iliacha gumzo kwa muda mrefu lakini kwa sababu ambazo niliziheshimu alisema asingependa iwe hivyo, uhuru wa kuwaacha watu watafsiri wao ndo raha ya kazi yake ingawa yeye anajua hasa kwanini alichora na maana yake hasa ni nini! Kwa heshima ya sanaa ilibidi nikubali matokeo. Toka umeanza kumjua na kufuatilia kazi yake, mara ngapi ushawahi kuskia Masoud yuko matatani? Yaani kakamatwa au hajulikani alipo? Kwangu mara kadhaa lakini haikuwahi kuwa kizuizi cha yeye kuacha kufanya afanyacho, kuogopa je? Nadhani kama binadamu kuwa na uoga ni jambo la kawaida, ila unafanyaje baada ya hapo ndo tofauti yetu.
Episode hii inajumuisha karibu yote ambayo niliwahi kutaka kumuuliza, mengine nilipata majibu nlotaka na mengine yalitolewa mbavuni, kwa ki vyovyote vile nili enjoy sana mimi na wenzangu na kutoka kwetu tunatumai nawe uta enjoy kama ambayo nasi tuli enjoy na kujifunza kutoka kwa MWAMBA huyu.
Love,
Salama.
Kuna mambo mengi wakati mwengine ambayo yanakua yanaendelea au yalitokea kwenye maisha ya baadhi ya watu ambao huja kukaa kwenye kiti chetu chakavu na meza yenye kigae. Ila kwasababu zilizo wazi za kuwataka wasijisikie uncomfortable na pengine kuwafanya hata ambao wangependa au ambao tungependa waje nao wasijiskie hivyo ndo kanuni ambayo tumeamua au niseme niliamua kipindi huko nyuma kuifuata. Nia na madhumuni ya session zetu hizi zaidi ni kuwapa watu maua yao wakiwa hai, sisi nasi kuskiliza hadithi za maisha yao ambazo zitatupeleka sehemu fulani katika maisha yatu na hili pia humuambia kila mgeni anapokalia tu kiti chetu chakavu kabla hata camera hajiwashwa ya kwamba… Sisi tuko hapa kwaajili ya kutaka ku inspire zaidi na si kumdhalilisha au kutaka kumuangalia kwa chini yoyote kwasababu tu kabla kuna kwikwi kadhaa zilishawahi kutokea kwenye maisha yake na tuka tumia hiyo kama ‘fimbo’ kumchapia nayo. Kama mwenyewe ana simulizi yake ya ‘majuto’ ambayo wengi wanaifahamu na haikumueka sehemu nzuri na angependa kuiongelea basi ruhusa ipo, ila kama ni kitu ambacho mwenyewe hayuko tayari kukiongelea basi kuheshimu hilo ni jukumu letu NAMBARI MOJA. Najua pengine inawezakana kabisa ukaona ah basi kuna haja gani ya kuongea nao then? Haja ipo na naamini tukipatacho hutosha, bila ya kuvunjiana heshima au kuwekana uncomfortable. Ukikua zaidi utaelewa zaidi .
Lulu Diva ni moja ya majina makubwa kwenye muziki wetu hapa nyumbani na pia kwenye kiwanda cha uigizaji, hustle zake za spidi KUBWA ndo ambazo zimemfanya awe anatambulika na mambo mengine kuweza kwenda vizuri kama jahazi kwenye hali ya hewa shwari huko baharini. Ila hayo yote hayakuja tu kwasababu labda yeye ni maalum sana, au mzuri sana au anajua kuimba sana, kiukweli wake, haya yamekuja baada ya jasho tele, mchozi tele na pengine damu kiduchu.
Jinsi alivyokua ilikua kwa malezi ya Bibi maana Mzee wake alikua na mambo mengi, Mama yake nae alikua akimpambania goli kama wengi ambavyo wamekua wakifanya kwa watoto wao. Kukua kwake kwa kiasi kikubwa ni Tanga na ananisimulia kwenye apisode hii jinsi ambavyo alikua akihama vijumba na maamuzi magumu ambayo aliyafanya yeye na Marehemu Mama yake ya yeye kuja TOWN. Lulu ananihadithia pia jinsi alivyokua akijituma ili aweza kumleta Mama yake mjini baada ya kuskia ameanguka kwa mara ya kwanza. Ni binti tu ambaye ndoto yake ilikua ni kuishi na Mama yake mzazi ambaye maisha hayakua hivyo wakati anakua. Ilikua inambidi afanye mambo kadhaa mpaka alipoweza kutimiza ndoto yake hiyo ya kumleta Bi Mkubwa hospitali kwa mara ya kwanza. Mengi yalitokea na ambayo yalikua nje ya uwezo wake ila kwa Rehema za Mwenyezi Mungu kadhaa aliweza kuyakamilisha ambayo kwa mujibu wa simulizi zake naamini Mama ametangulia mbele ya Haki akiwa na roho safi kwa Binti yake.
Story ya Mama Lulu ndo ambayo kwa kiasi kikubwa ilibeba mazungumzo yetu haya, ingawa pia kwa ki upekee kabisa tumeweza kuzungumzia mahusiano yake, kazi zake, ndugu zake, maisha nyuma ya camera , kazi zake, uandishi, muziki na filamu na hakua mchoyo wa kujielezea na kutuelezea hata kidogo. Yangu matumaini pia nawe utaskiliza na kuitimaza kwa MAKINI na kwa kiasi fulani utaweza kuelewa baadhi ya mambo ambayo yatakufanya hata ukimuona uwe na heshima fulani kwa Binti huyu.
Tafadhali Enjoy.
Love,
Salama.
Doris Mollel kwa kuanzia tu tuanze na jina lake, ni zuri lenye kukumbukwa ki rahisi, yeye mwenyewe pia ni mrembo na mkarimu, sana. Roho yake ni kama rangi yake, nyeupe na kwa bahati Mimi namfahamu yeye kiasi kwa kupitia rafiki zangu ambao yeye anafanya nao kazi na pia ana mahusiano nao mazuri, sana. Pia namfahamu mume wake ambaye tukianza shindano la kumtafuta nani mkarimu kati yao tunaweza kukamaliza kwa suluhu. Huwa naamini Mwenyezi aliwakutanisha ili kwa pamoja waweze kufanya makubwa kwaajili yao na familia zao na jamii ambayo imewanzunguka ambayo kwa kiasi kikubwa ina uhitaji wa yale ambayo wao wameyaona wanaweza kufanya jambo ili yawe mepesi.
Sasa tuanze kwa vipi Doris amekua akifanya ambayo anayafanya sasa ambayo baada ya kufanya kipindi hiki mengi ambayo aliyaongelea kama ya Serikali ya Uganda kumpa tuzo na kumkaribisha nchini mwao ili aweze kushirikiana nao bega kwa bega kwenye suala zima la kuwaokoa watoto wanaozaliwa kabla ya wakati yaani ‘NJITI’ na hivi karibuni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia S. Hassan kutoa MILIONI 70 kwaajili ya kuchangia mfuko wake wa Doris Mollel Foundation. Yeye alikua anataka tu kufanya kitu kwaajili ya kuisadia jamii yake, ananiambia wakati analizungumzia hilo huku akitafuta jambo la kufanya ndipo Mama yake alipomfugua macho kwa kumuambia masuala ya watoto njiti, taa iliwaka sasa baada ya Mama yake kumkumbusha kwamba hata yeye alizaliwa kabla ya wakati. Alipoambiwa hivyo hakukua na kurudi nyuma tena baada ya hapo.
Ananisimulia vikwazo ambayo aliwahi kupata mwanzo kuanzia nyumbani mpaka kwenye kutafuta hizo pesa ambazo zinasaidia mpaka leo hii, Doris ananihadithia jinsi ambavyo alipata bahati ya kuwa na watu ambao wamemsapoti na wanamsapoti mpaka leo kuanzia nyumbani kwa mume wake. Mtu ambae ndoa yao ilikua changa kuanza kuwa na vikao na watu mbali mbali mpaka usiku wa manane inamtaka mtu muelewa sana kuweza kuamini na kuyaacha mambo yaende. Mumewe alikua huyo mtu. Kwa ambao walimpigia simu mara ya kwanza baada ya kuona anchojaribu kufanya, watu kama Asas wa kule Iringa na wengine ambao wamekua wakijitokeza siku baada ya siku. Anakumbuka na anajua kwamba kutokata tamaa kwasababu ya changamoto kadhaa ndo ambapo kunamfanya awe ni mmoja ya watu wanao heshimika zaidi kwa mchango wake kwenye jamii yetu.
Binafsi naamini huu ni mwanzo tu wa mazuri mengi ambayo binti huyu halisi wa ki Tanzania anajaribu kufanya. Sekta ya kulea watoto ambao wamezaliwa kabla ya wakati inahitaji hela nyingi na kwasababu ambazo Mimi na wewe hatuzijui kumekua na vifaa VICHACHE sana vya kuwahifadhi watoto hao mara tu wanapo zaliwa. Doris na Foundation yake amekua akipigana vita hiyo kuhakikisha vifaa vinapatikana sio mjini tu, hata mikoani ili kuokoa maisha ya watoto hawa ambao wengine huishia kwenye debe la taka kwasababu tu walizaliwa kabla ya wakati wao.
Yangu matumaini utamuelewa na utapata nafasi ya kumfuatilia na kama utakua na lolote ambalo unaweza kuchangia basi yuko kwenye mitandao ya kijamii maana siku hizi kumpata mtu na kujua ambacho anakifanya imekua rahisi kupitia mitandao hiyo. Mimi najivunia sana yeye na yangu matumaini atafanikiwa sana kwenye sekta hii kama nasi tutaweza kumsaidia pale panapowezekana.
Tunahitaji kina Doris tele kwenye jamii yetu maana vya kusaidia viko vingi.
Yangu matumaini episode hii itasaidia kukufungua macho kwenye mengi ambayo jamii yetu ina uhitaji.
Love,
Salama.
Nilipoandikiwa ujumbe mfupi na Edwin Bruno ambaye ni mkwe wa Professor kwamba Mama amekubalia kufanya kipindi na sisi siku hiyo ya Jumapili akishatoka church nilihisi kama naota. Mwenyezi Mungu anajua kwa kiasi gani tumekua tukitaka kufanya maongezi nae kwenye kipindi chetu. U busy wake na pengine mara nyingi kutokuwepo Dar es Salaam napo palikua panaleta ugumu, nyengine ilkua ni tarehe zetu za kufanya production na availability yake zilikua zinapishana sana. So unaweza ukaelewa excitement ambayo nilikua nayo baada ya finally samaki kujaa kwenye ndoana.
Professor Anna Tibaijuka ni LEGEND miongoni ma magwiji kwenye nchi hii kwa kazi yake na usomi wake na uzazi wake na kujibeba kwake. Kazi mbali mbali ambazo amewahi kuzifanya na kuliwakilisha Taifa hili zinajizungumza kwa sauti kubwa. Ila Safari yake mpaka anafikia kwenda kufanya kazi kwenye Taasisi kubwa duniani hakukumdondokea tu miguuni. Usomi wake ambao aliupambania toka akiwa mdogo na kupata ushirikiano kutoka kwa Marehemu Baba yake ndo kila kitu. Enzi ambazo mtoto wa kike alikua anaandaliwa kuwa Mama wa nyumbani, Baba yake aliamini zaidi kwenye kumpeleka mtoto wake shuleni na kwa mujibu wa Mama Tibaijuka Baba yake alikua aliwasisitiza wazee wenzake kufanya hivyo maana dunia ndo ilikua inaelekea huko, kuna ambao walimsikiliza na wengine ambao waliona anapoteza tu pesa na muda.
Mama Tibaijuka na Mimi tuliongelea kuhusu gharama za elimu enzi hizo Mimi nikidhani elimu “ilikua bure” pasi na kujua elimu kipindi hiko ilikua ghali pengine kuliko sasa na ukichukulia shule zenyewe zilikua mbali kweli kweli. Ananiambia pia suala la yeye kutaka kutomuangusha Baba yake ambaye baadhi ya watu walikua wanamcheka kwa kumpeleka Anna shuleni na kuingia gharama zote hizo. Pia ananiambia kuhusu Mama yake kufanya kazi zaidi ili masuala ya nyumbani aweze kuyafanya yeye ili kumsaidia mumewe ambaye pesa yake karibia yote alikua akilipia elimu ya Binti yake.
Mama Anna pia ananisimulia humu jinsi ambavyo aliposwa alipokua kidato cha tano na mchumba ilibidi amsubiri mpaka alipomaliza Chuo Kikuu. Nili enjoy kila sekunde ya maongezi haya ambayo kwa kiasi kikubwa naamini yatakua na faida kwetu sote. Ananihadithia pia jinsi ambavyo alienda Sweden na mumewe ambayo alikua huko kikazi na jinsi ambavyo alipata nafasi ya kusoma Chuo Kikuu BURE na ni nafasi ambayo aliipokea kwa mikono miwili na kuhakikisha hafanyi makosa.
Mama Anna ameshaifanyia Dunia hii mambo tele ya kimaendeleo wakati akifanya kazi zake UN na baada ya hapo alirudi nyumbani na kukifanya kazi Chama cha Mapinduzi kama Mbunge wa Muleba Kusini na Waziri wa Ardhi, nyumba na Maendeleo ya makazi. Hapo kwenye uwaziri sasa… Kulikua na mengi yaliyotokea wakati yeye yuko kwenye cheo hiko na ambayo kwa ki ufupi tu tuliyajadili kwenye meza yetu. Mama Anna yuko na Respect ya hali ya juu kwa Rais wa awamu ya nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ambaye kwa kiasi kikubwa alimfanya Professor Tibaijuka arudi nyumbani na kulifaidisha Taifa na yale alojifunza wakati anafanya kazi huko kwenye Umoja wa Mataifa.
Yangu matumaini utaokota kadhaa kwenye maongezi yetu haya na kwa kiasi flani yatakusaidia kwenye maisha yako. Tafadhali enjoy pia.
Love,
Salama.
Katika pita pita zangu siku si nyingi nilimsikia mtu akimzungumzia mgeni watu wa wiki hii kwamba ni ‘Jay Z’ wa Bongo na si kwasababu kamuoa mmoja wa wasanii hodari wa kike na ambao wako juu ki muziki, ila pia akili yake ya kibiashara kwa kiasi kikubwa imemfanya yeye aone hivyo. Kwa ufahamu wangu niliambiwa na kushuhudia suala la maneno na mawazo ‘kuumba’. Pale mtu au watu wanapo kuona na ukichanganya na juhudi zako na nia na madhumuni ya wewe kutaka kufika pale basi mengine kutimia huwa ni suala la wakati tu.
Hivyo pia ndivyo ambavyo mimi namuona Ndugu William Nicholaus Lyimo almaaruf Bill Nass. Mara yangu ya kwanza kukutana nae uso kwa macho ni miaka kama sita au saba iliyopita wakati nafanya kipindi cha Ngaz kwa Ngaz special edition. Ambacho mimi na Josh Murunga tulikua tunafanya ilikua kuwapa nafasi wasanii hodari kuwa ma host wa countdown hiyo ya ngoma zao kali 20 kwa wakati huo na kuzitolea maelezo yake. Kwa Bill Nass ilikua kama kumtafuta Kuku tu, yaani RAHISI sana. Alikua natural wataalam wanasema, kuanzia matamshi (haya wengi huwashusha hadhi kwa kiasi flani) mpaka swagg ambayo mtangazaji anatakiwa awe nayo kwake ilikua ipo. Kuvaa kwake, kuheshimu wakati na kuskiliza maelekezo na kisha kuyafanyia kazi ilikua 100, na mimi kwenye hili nilikua mtazamaji tu, kazi kubwa aliifanya Ndugu Josh akiwa kama Director. Yangu matumaini Bill Nass siku moja atataka kufanya kitu kama kile maana kitamfaa mno na itakua moja ya income zake nyingi ambazo anazo.
Kwake yeye kuamua kumuoa mmoja ya wasanii hodari wa kike ambaye ana mashabiki wengi na pengine wengi wao ni wanaume nadhani lilikua si amuzi mdogo kwao wote wawili. Wawili hawa mahusiano yao yalikua hadharani kwa sote kuyaona na kuwa na maoni nayo. Kuanzia ku leak kwa video yao ya faragha mpaka mahusiano ya mkewe na Marehemu Ruge, kila kitu kilikua nje nje. Je haya yaliathiri au kuyajenga mahusiano yao kwa kiasi gani?
Vipi kuhusu suala la Marehemu Godzilla ambaye kulikua na shutma kwamba alikua anauiga style yake na baadhi ya Radio zilikua zinampa nafasi yeye ili kumficha Zilla? Na je suala la kifo chake ambalo lilimleta yeye karibu na mtoto wa Zilla? Hii ilikua inamsumbua vipi wakati watu wanasema hivyo? Na je alikua anaona jinsi ambavyo ilikua inamsumbua Zilla?
Ukiachana na muziki Nenga pia ni mfanyabiashara mzuri tu ambaye amekua akitumia jina lake ipasavyo ili kuweza kujitengenezea kipato cha pembeni ambacho ni cha uhakika zaidi kuliko mziki ambao anafanya. Nna uhakika na yeye anajua kwamba ana uhakika wa kuuza electronics zaidi kwa mara nyingi kuliko uhakika wa kuwa na hit song nyingi kwa mwaka. Na hiyo haimaanishi kama yeye si msanii HODARI ila zaidi kwenye suala la wimbo kuwa mzuri lakini watu wasiupokee kama matarajio yanavyokua.
Humu pia tulichambua kiasi kuhusu jina lake ambalo amelirithi. Majukumu, biashara, mapenzi, urafiki, usia na familia.
Ningependa u enjoy kama ambavyo sisi tu enjoy wakati tunaongea.
Love,
Salama.
Ushawahi kuwa na mtu ambaye mnafahamiana vizuri miaka nenda na miaka rudi na hata pengine kwa u busy wa maisha zikapita siku hamjaongea lakini unajua yuko sawa yeye na Familia yake na mambo yanaenda vizuri, na kama isingekua hivyo basi ungekua ushajua? Ambaye unajua kukiwa na situation flani basi yeye anatafanya jambo flani na kuzima au kuwasha moto, na kama kuna neno umeambiwa kasema unajua kabisa ni kweli au si kweli? Au kama una suala unataka kulifahamu vizuri linalohusu mambo fulani na jibu ambalo atakupa yeye ni la 100 na hatapindisha hata kidogo? Basi huyo ni Carol Moses Ndosi kwa Salama Jabir yangu.
Lini tulikutana? Yoh 😃! Wakati sote tunafanya kazi IPP Media,Carol alikua rafiki wa Tabea Kaduri ambaye alikua nae kwenye channel ya kiingereza ya 101.4. Si unamjua Carol na kizungu? Then ITV then EATV, mimi na Carol tukaja ku click zaidi kwasababu tabia zetu nyingi (za ujana) zinafanana. Pia tulienda wote Makongo Secondary School ingawa mimi huko simkumbuki maana mambo yangu yalikua mengi kiasi. Pia mimi ni Dada yake ki umri. Kuna story moja ya Carol ya kujifunza gari bila ya kunipa taarifa. Siku moja kaibuka tu ITV nje na kuniambia twenzetu kwa Kiula huku yeye ndo suka bila ya kujua lini hasa alijifunza kuendesha hilo gari! Nadhani hii ni moja ya memory nzuri kati yetu. Ukiachana na kwenda Chang’ombe kumfuata Steve Mbobo na gari letu ambalo AC Mungu ndo anajua,foleni ya Keko na sisi ilikua inafahamiana vizuri. Tumeishi na tunaendelea kuishi Alhamdulillah, na mambo yetu? Ah mambo yetu Allah anaendelea kuyabariki sana. Tunashkuru kwa kweli.
Kukua sasa ndo huku, kila mmoja kajiajiri kwa kuyafanya yale aliyo jichagulia. Carol kama wengi mnao mfahamu na ambaye humu kwenye maongezi yetu ya kwenye kiti chakavu na meza ya kigae yatakufanya umfahamu zaidi kwamba ni JEMBE. Mpambanaji kabisa ambaye nae kama binadamu mwengine wakati mwengine humfika hhaapa na pengine kutaka kukata tamaa. Lakini uzuri ni kwamba ana nguvu na kiu ya kutaka KUENDELEA na KUSHINDA, pengine hiyo ndo silaha yake NAMBARI WANI. Kwa utashi wake ameweza na anaendelea kuweza kuwafunza mambo wengi wetu juu ya masuala ya ki mtandao na kujielewa binafsi. Wakati wa Nyama Choma Festival Carol na kikosi kazi chake aliweza kufanya kazi iliyo tukuka ambayo ililifanya tamasha hilo liwe ni moja ya matamasha BORA kabisa ambayo yashawahi kutokea hapa Tanzania. Mitihani ambayo aliwahi kukutana nayo wakati tamasha hilo likiwa linaendelea ambayo mengine ilikua ya Mungu na mengine ya Binadamu ni Carol mwenyewe na team yake ndo ambaye anaweza kuelezea na kwa kiasi kiduchu sana, amegusia kwenye maongezi haya.
Heshima zangu kwake anazifahamu ingawa wakati mwengine tunakubaliana kuto kubaliana kwenye baadhi ya mambo lakini urafiki na u Ndugu wetu utabaki pale pale. Mimi na yeye tushafanya mengi, tushaona mengi, tushajifunza mengi na bado tunaendelea kufanya hivyo. Na nia hasa na madhumuni ya episode hii ilikua kutaka wewe unafahamu Ndugu yangu huyu zaidi. Na ningetamani sana kuweza kuyaweka wazi yooote na majina yake ila kwa staha na heshima, kwa leo tuishie hapa.
Yangu matumaini kama kawaida utaokota mawili matatu ambayo yatakusaidia kwenye safari na vita zako binafsi.
Keep going.
Love,
Salama.
Lameck Ditto Sr ni Baba, Mwalimu, mwanamuziki, muandishi, mentor, mume na zaidi ya yote ni mwana tu ambaye maisha alopitoa kipindi anakua hayajawahi na wala hayatawahi kumsahaulisha yeye ni nani na wapi ambapo ametokea na wapi anataka sana kuelekea maana huko ndo kwenye kesho yake, na kwa kumsikiliza ambavyo nimemsikiliza, kesho yake anaithamini sana na amekua akiiandaa vizuri ili hata siku moja asije akakwama na kuanza kuishi maisha ya jana ambayo yalikua si mazuri hata kidogo.
Yeye na Baba yake mzazi walikutana kwa ‘bahati mbaya’ tunaweza tukasema hivyo maana wakati yuko zake Morogoro akiendelea na maisha ya kuishi yeye na Kulwa huku wakijilea wenyewe, Ditto au Dotto ananihadithia vile ambavyo Rafiki yake aliweza kumkutanisha na Mzee wake bila ya yeye kutegemea.
Alikua ananiambia vile ambayo ilikua inabidi apambane kupata ya kula na pa kulala baada ya kuja jijini Dar es Salaam na haya yote ni baada ya yeye tayari kuwa umeshatoka na WATU PORI enzi hizo na hapo pia ni baada ya kupata nafasi ya kurekodi album moja na producer PFunk enzi hizo, PFunk huyo huyo ambaye alikua akilitikisa TAIFA kwa kazi nzuuri alizokua akifanya na wasanii kadha wa kadha ikiwa pamoja na Juma Nature.
Lameck anakumbuka jinsi alivyokua analala ndani ya kiduka kidogo cha mwanawe mmoja ambaye alishamsomesha ili amstiri ki hivyo, alivyokuja Dar alikua anakaa kwa mwanae mmoja ivi na mkewe ila baada ya ahadi za album kutoka na kwamba mambo yatabadilika kugonga mwamba, Lameck ilibidi atafute ustaraabu mwengine.
Nilitaka kujua kama hiyo ndo ilikua lowest moment ya maisha yake? Au kifo cha Mama yake? Au Mamu kukataa album yake kwa kusema haikua na kiwango kile?
Sasa ni Baba na mchumba wa muda mrefu wa Binti mmoja ambaye nae alikutana nae ki ajabu ajabu tu na ambaye pia alimzungusha sana kabla hajanasa kwenye ndoana. Baba wa mtoto ambaye Mimi baada ya kukufanya nae mazungumzo nilikutana nae uwanjani akiwa ameenda kumuangalia Lameck Jr akifanya yake kwenye moja ya mechi za soka za shule ambayo anasoma. Kwenye meza aliniambia moja ya ahadi ambazo amejiwekea ni kuhakikisha yuko pale kwaajili ya mtoto wake, jambo ambalo yeye hakuwahi kulipata mapema.
Mwanzo nilikuambia yeye pia ni muandishi, muandishi wa mashairi ya muziki na pia ni muandishi wa matangazo, kazi ambayo anasema Marehemu Ruge Mutahaba ndiye ambaye kwa kiasi kikubwa alimuelekezea huko. Na mentor wake mwengine ni Ndugu Ruben Ncha Kalih ambaye kwa asilimia KUBWA amempika na akapikika.
Tulizungumzia pia umuhimu wa mmoja kuwa na chanzo zaidi ya kimoja cha kupata pesa, kuweza kukabiliana na MSIMU ambao unakua huna wimbo (au kazi) lakini bado ukaweza kuishi, kuhusu maamuzi ya yeye kwenda THT wakati tayari alikua ARTIST ambaye ameshajijenga. Tuliongea pia kuhusu Ruge, Barnaba, Amini na mambo mengine tele. Binafsi nilikua na wakati mzuri sana wakati tunaongea haya na yangu matumaini itakua hivyo kwako pia.
Tafadhali enjoy.
Love,
Salama.
From the publisher's feed