Salama Na

Salama Na

Download on the App Store

Salama Na episodes

  • SE7EP18 - SALAMA NA FAROUK KAREEM | SAILOR

    Hii nayo ni moja ya zile ambazo ziliuliziwa sana na kwa muda mrefu nasi kwa upande wetu tumekua tukiifukuzia tuweze kukaa na mwamba huyu hodari kutoka Zanzibar. Mimi mwenyewe ambaye nimekua nikifanya kazi kwenye kiwanda hiki cha burudani nilikua na hamu ya siku moja kuwa kwenye meza moja na Ndugu yangu huyu, kuweza kumtazama usoni na kumuuliza yote ambayo nilikua nataka kumuuliza kwa kipindi kirefu sana. Maana hata mimi nimekua nikimsikiliza miaka nenda miaka rudi na siku zote emeemdelea kutuhabarisha kwa sauti ile ile na spidi ile ile. Ukiskia mtu ameweza kuwa bora toka siku ya kwanza basi moja ya mifano hai ni Farouk Kareem wa ITV na Radio One. Nikiwa mzanzibari wa kuzaliwa, Farouk amekua ni moja ya watu ambao nimekua nikiwaskiliza na kuwaheshimu sana. Mchango wake kwenye tasnia ya uwandishi wa habari na kuziripoti habari hizo Taifa zima unalijua, toka enzi zile za kipindi cha Spoti Leo cha Radio One ambacho yeye alikua alishiriki kama reporter kutoka Zanzibar na baadae na yeye akajiingiza katika kinyang’anyiro cha kugombea nafasi ya uongozi kwenye Chama cha Mpira cha Zanzibar yaani ZFA na akapata na katika watu ambao walipiga kazi iliyo TUKUKA enzi hizo na ambayo iliacha alama basi Farouk ni mmoja wapo. Nani aatasahau kama moja ya idea zake ilikua ile ya kutaka Zanzibar iwe na kiti chake kwenye Shirika la Mpira la Afrika na la Dunia yaani CEFAFA na FIFA. Farouk Kareem alikua ndo injinia wa kutaka hilo LIWEZEKANE. Mtoto wa kwanza kwenye familia ya watoto wawili tu na wote wa kiume, Farouk Karim ni Kaka wa mmoja kati ya ma Pilot hodari na wa muda mrefu ambao hii nchi imeshawahi kuona ambaye na yeye sasa ana mtoto pia ambaye naye ni Rubani. Kaka huyo Kapten Arif Jinnah na mwanawe First Officer Amour Arif. Ki ufupi familia yao imejaa watu wa kazi kabisa. Naamini si wengi ambao tulikua tunayajua mahusiano hayo ya wawili hawa ambao kila mmoja wao amekua akiandika historia yake kwa upande wake. Farouk ni Baba wa watoto kadhaa wa Kike ila miaka si mingi sana Allah pia nae kampa mtoto wa kiume. Kwenye episode hii tumezungumzia familia na majukumu, tumezungumzia jinsi mmoja anavyoweza kutafuta kwa njia zake na wazazi nao wakitoa baraka zao basi hakuna ambalo linaweza kushindikana kama tu nia na madhumuni yapo. Anakumbuka jinsi ambavyo alimaliza skuli na kisha akawaambia wazazi wake kwamba yeye anataka kuwa BAHARIA na wao WAKARIDHIA. Anasema kipindi hiko kulikua na wimbi la ma Seaman tele ambao walikua wakirudi likizo nyumbani Zanzibar wanakua wako ‘vizuri sana’ na hiyo ni moja ya mambo ambayo yalimvutia sana. Na wazazi wake waliridhia na kuhakikisha kijana wao anatimiza ndoto zake kwa kumuwezesha. So, kwenye habari nako alifikaje? Hii ni moja ya episode nzuri sana ambazo nimewahi kufanya msimu huu na yangu matumaini nawe uta enjoy kama ambavyo sisi tuliburudika wakati wa mahojioani haya. 

    Love, 

    Salama.

    1 hr 24 min
  • SE7EP17 - SALAMA NA ROSE MUHANDO | NIPE UVUMILIVU

    Katika binadamu ambao walinipa wakati mgumu na kusubiri kwingi kabla ya kuja kukaa kwenye meza yetu ya kigae na kiti chakavu basi mmoja wao ni Rose huyu wa Muhando. Upatikanaji wake ni kama ukitaka kumuona SIMBA mbugani, lazima uamke asubuhi na mapema au uwe na bahati ya mtende kama ambayo sisi tumepata. Ingawa tulisubiri kwa masiku tele na miezi tele katikati ya mwaka huu tuliweza kumpata na kukaa nae chini ili tuweze kuzungumza nae.

    Rose ni wa moto sana, kalenda yake imejaa safari tele za nje na ndani ya nchi, anazunguka mara kwa mara kwaajili ya kutoa elimu na burudani kwa watu wengi ambao nao pia wamekua wakimgojea kwa hamu na kwa masiku tele. Kipaji chake cha kipekee ndicho ambacho kimemfanya awe maalum miungoni mwa wasanii wanaofanya muziki wa Injili na uzuri wake mwengine ni kwamba amekua akitoa huduma hiyo kwa miaka mingi bila ya ‘kuchuja’.

    Sasa nini hasa siri ya mafanikio hayo?! Ukiachana na panda shuka tele ambazo Rose amepitia toka akiwa na umri wa miaka 6, kukata tamaa ni jambo ambalo halipo kabisa katika mambo ambayo huwa anayawaza. Pengine kujiuliza kwanini na anatokaje kwenye hilo zito alilo nalo linaweza likawa ndo swali, ila kusema kwamba hatoweza au haiwezekani hilo jambo kwenye kitabu chake au kichwani chake huwa halipo kabisa.

    Ukiskiliza kwa makini maneno ambayo yanatoka katika mdomo wake utagundua Rose ni mmoja kati ya wanawake jasiri sana ambao wamewahi kutokea katika kiwanda hiki cha Sanaa hapa Tanzania. Ukimuangalia macho yake, mikono yake ambayo imejaa makovu na nna uhakika pia kuna sehemu nyengine kwenye mwili wake pia zimejaa makovu lakini hatukuweza kuona unaweza ukapata tu idea ya makubwa na mazito ambayo amepitia na ambayo yameacha makovu makubwa tu si mwilini mwake tu bali hata kwenye moyo wake. Ananihadithia kwenye episode hii jinsi ambavyo watu walikua wanamuadhibu ki mwili na ki akili ikiwa ni pamoja na kupigwa, kuchomwa moto, kukatwa na kunyang’anywa mali zote ambazo amewahi kutengeneza tokea wakati anaanza muziki ila hayo yote hayajawahi kumkatisha tamaa wala kumrudisha nyuma.

    Rose anaamini na aliamini kwamba ana uwezo wa kuvipata vyote ambavyo watu walimdhulumu kwenye kipindi flani kwenye maisha yake, aliamini hakuna ambaye anaweza kumnyang’anya kipaji ambacho Mwenyezi Mungu amempatia na kwa kupitia hiko kipaji na akiwa hai na mzima basi vyote ambavyo aliwahi kuwa navyo na vikapotea basi alikua na uwezo wa kuvirudisha na ni kweli, kuvirudisha ameweza na vimekuja maradufu yake.

    Simulizi zake za safari yake toka siku ya kwanza alipokua mdogo nyumbani kwa Baba na Mama yake huko kwao Morogoro wakati anaumwa ni moja ya vitu vya kufikirisha sana ambavyo nimewahi kuvisikia toka tumeanza kukalia kiti chakavu, na yangu matumaini maongezi haya kwa kiasi kikubwa yatakupa ile vibe ambayo huwa naizungumzia kwenye intro ya kipindi chetu hiki.

    Tafadhali enjoy.

    Love,

    Salama.

    1 hr 21 min
  • SE7EP16 - SALAMA NA ZAHIR ZORRO | KIMULIMULI

    Zahir Ally Zorro ni mkongwe wa muziki wa dansi na kwa habari ambazo nimepata ni kwamba enzi zake alikua wa moooto sana tena kwenye kila nyanja, kuimba, kuandika, kupiga gitaa na mpaka uvaaji, alikua handsome boy sana na ulimbo kwa kina Dada enzi hizo. Utashi na ucheshi na u sharp wake ndo ambao ulikua unamfanya asimame PEKEE kwenye kadamnasi ya wanamuziki wengi wa kipindi hiko. Naomba nikukumbushe pia kwamba enzi hizo zilikua pia si za kuzichukulia poa kabisa, maana ushindani wa bendi na vipaji binafsi ulikua wa hali ya juu sana, na yeye kama yeye alikua moja ya wale WAKALI wa kipindi hiko. Kama muajiriwa wa Jeshi Mzee Zahir alikua shujaa wa aina yake enzi hizo za ujana wake, kama askari alikua akijituma na ndo maana hakua na cheo cha kinyonge, na kama muandishi na muimbaji na mpiga gitaa pia alikua na nafasi yake ya kipekee. Ukimuangalia hata rangi yake imekaa ki chotara na kwenye mazungumzo haya ana nikumbushia jinsi ambavyo Baba na Mama yake walikutana na ambavyo yeye alizaliwa. Interest yangu zaidi ilikua jinsi ambavyo yeye kama Baba ameweza kuwakuza watoto wake wawili ambao nao wamekuja kuwa wanamuziki wazuri tu tena, Marehemu Maunda Zorro ambaye alifariki mapema mwaka huu (Mwenyezi Mungu amsamehe makosa yake na Amrehemu) na Kaka yake Banana Zorro. Wakati wa kuanza Banana ndo alionekana kuwa angekua super star zaidi ila Maunda nae alipoikamata reli yake kila mtu alimfahamu vizuri. Malezi yao baada ya Marehemu Mama yao nae kutangulia mbele ya haki wakiwa bado wadogo naamini ilikua mtihani mkubwa kwa Mzee Zorro. Ila kwa Rehema za Mwenyezi Mungu Mzee huyo aliweza na ameweza kuhakikisha watoto wake wanakaa kwenye mstari ulio nyooka na kufanya mziki mzuri na kwa heshima na taadhima. Kwenye maisha yangu ya kazi hii nimeshawahi kukutana na Mzee Zorro ila hatukuwahi kufanya maongezi kama haya ingawa nyuma ya ubongo wangu siku zote nilikua nataka kufanya hivyo, na wakati mwengine nilikua nawaza hata ingekua viti VITATU upande ule yaani Baba na watoto wake wawili, kisha nikaona tutakosa kinaga ubaga nyingi, yaani hatutawafaidi sana kama tukiamua kufanya hivyo maana kati ya watatu hao kila mmoja ana story zake ambazo anafaa kupatiwa wasaa wake. Kwa bahati mbaya Maunda alitangulia mbele ya haki na wakati kwa upande wetu ulifika kwa sisi kutaka kukaa chini na Mzee Zorro ili tuyajue yake na kutaka kujifunza kutoka kwake. Mimi na Director wangu wa episode hii tulikua na wakati mgumu kiasi maana pengine tulitaka zaidi ya ambacho tuliweza kupata na hilo Mimi na Alex (Director wangu) tumekubaliana kwamba imetokana na kuondoka kwa Maunda, tunaamini toka Maunda amefariki Mzee Zorro hajarudi katika hali yake ya kawaida, na inaeleweka maana yule hakua tu Binti yake, alikua ni rafiki yake wa karibi saaaana pia. Mzee Zahir alikua analala na Maunda na Banana chumba kimoja mpaka siku chachu tu kabla ya Maunda kukua, na hiyo ilikuja baada ya Banana kumuambia Mzee wake kwamba pengine sasa umefika muda wa wao kulala tofauti. Ananiambia katika episode hii kwamba yeye waala hakua anaona tatizo lolote juu ya hilo maana wenyewe walikua wanaishi tu kwa upendo na maelewano ila baada sasa ya Banana kusema ndo hata yeye alipoona ni kweli muda wa kupeana faragha kwa kila mmoja kuwa na sehemu yake ulikua ushafika. Kwa mtu ambaye walikua wanaonana karibu kila siku na kuongea sana hata baada ya Maunda kuhamia kwa mtu wake ukaribu wao bado ulikua wa karibu sana. Mimi namuombea Mzee Zahir Ally Zorro wepesi katika kipindi hiki kigumu ambacho anapitia na In Shaa Allah arudi katika hali yake ya zamani ya ucheshi na bashasha tele na kwa hii ambayo tumeweza kufanya naye itakupa ufahamu wa kiasi wa legend huyu ambaye pia ni mjuzi wa mambo mengi ya historia na muziki wa jana na wa leo hapa ulimwenguni, ukitaka kuongea na Mzee Zorro hukusu culture ya Mexico, mabadiliko ya tabia nchi, timu ya Taifa ya Ufaransa, mapenzi ya Tabu Ley na Mbilia Bel yote atakua na la kukuambia. Special special human being.

    Tafadhali enjoy. 

    Love,

    Salama.

     

    52 min
  • SE7EP15 - SALAMA NA MCHUNGAJI RICH BILIONEA | SERMON

    Kipindi cha nyuma kidogo nilifanya lile ambalo huwa nafanya la kuwashirikisha rafiki zangu na team kuhusu list ya watu ambao wangependa kuwaona kwenye kiti chetu chakavu na sababu za kwanini hasa waje kwenye meza ile yenye kigae kwa juu maana tukisema tutaje majina tu bila ya sababu thabit za wao kuja pale tunaweza tukaondoa maana yenyewe ya kuwa na watu wenye story za kuvutia na kutufunza kama ambavyo tumekua tukifanya. Jina la mgeni wetu huyu lililetwa kwangu na Michael (Mx) Mlingwa na Ndugu yangu Elbogast Myaluko ndo alinipatia mawasiliano naye na kuanzia hapo mengine yamebaki kukhadithiwa kama hivi.

    Sikua namfahamu Mchungaji Richard Hananja mpaka Michael alipo niambia nami nikachukua muda wangu wa kwenda kufanya ka research kangu kabla hajaja mezani, ambacho nilijifunza ni kwamba Mchungaji alikua ni mtu mashuhuri sana ambaye ana watu wengi sana pia wanao mskiliza. Ilinichukua takriban miezi miwili kuweza kumpata maana kila weekend (mara nyingi rekodi za kipindi huwa zinafanyika weekend) yeye huwa yuko safarini. Huitwa sana sehemu mbali mbali, na sasa Serikali nayo imekua ikimuita pia katika matamasha na mikutano mbalimbali. Kwahiyo mara utamsikia yuko Dodoma, mara Moshi, mara Iringa ilimradi yuko busy. Na wakati mwengine Jumapili yake inakua ya yeye kualikwa kwenye Makanisa mbalimbali ili akatoe neno, siku hizi yeye ameshastaafu kuhubiri kanisani na sasa zilizobaki ni hizo za mialiko maalum.

    Kama kawaida mimi na wenzangu tulitaka kuanza kwa kumfahamu mgeni wetu maana kama nilivyokuambia hapo awali mimi sikua namfahamu zaidi tu ya kumuona kwenye mitandao akimwaga cheche, tulianzia kwenye kuzaliwa kwake na kukua kwake, mitihani mbalimbali ya ujana, bishara na kazi ambazo ashawahi fanya, na wakati naandika hii nimejifunza pia kuwa Mchungaji hana ambalo anaongeza chumvi maana baada ya sisi kufanya nae maongezi haya, nimeona ameenda sehemu tofauti tofauti na story yake haijawahi kubadilika.

    Ujasiri wa ziada huhitajika ili tuweze kufanikiwa kwenye maisha yetu na pia kuwa kwenye mstari ili usiingie kwenye matatizo na vyombo vya sheria. Mchungaji ananiambia jinsi ambavyo alikua ana hustle kila kona, kusafiri bila ya kibali cha kuvuka mipaka ya nchi na boxing ambayo aliifanya kwenye kipindi flani kwenye maisha yake. Boxing imemuachia kovu ambalo kila siku linamkubusha mapambano ambayo ameshawahi kuyafanya kwenye maisha yake.

    Boxing pia ndo ambayo imemfanya awe na discipline ya hali ya juu. Kwenye maisha yake ya sasa Mchungaji Hananja anatoa nafasi kwa kila aliye kata tamaa au ambae watu wamemkatia tamaa, yeye ndo huwachukua hao na kuwapa nafasi nyengine kwenye maisha yao, na amini usiamini wengi wao hunyooka na kuanza upya. Kwenye nyumba yake huko Madale Mchungaji anafanya mambo mengi ikiwa pamoja na kilimo na ufugaji. Swali langu lilianza kwa kutaka kujua hizo pesa za yeye kuweza kufanya mambo yote hayo, huwa zinatoka wapi?

    Mchungaji Hananja ni MUME, na kwa mujibu wa maelezo yake, alichelewa saana kuoa na mkewe ni Rafiki yake wa kwanza. Yangu matumaini moja mbili tulizopiga humu zitakupeleka sehemu.

    Tafadhali enjoy.

    Love,

    Salama.

    1 hr 6 min
  • SE7EP14 - SALAMA NA COACH EVARIST | FIRST QUARTER

    Evarist Mapunda ni moja wa makocha wangu wa maisha haya ninayoishi sasa hivi, ananifahamu toka nikiwa na miaka 17 mpaka sasa hivi ingawa hapa katikati baada ya ‘kuwa mkubwa’ nilipoteana nae kwenye mahangaiko ya kujitafuta na kutafuta maisha. Ila Mimi na yeye tunajua kila mmoja wetu ni mtu wa aina gani na anamaanisha NINI kwa mwengine.

    Ukiwauliza watoto na wakubwa wengi wa Upanga watakuambia nini yeye pia anamaanisha kwenye maisha yao, lazima atakua na simulizi kuhusu mwalimu huyu hodari wa basketball na maisha, kama hadithi hiyo itakua haimhusu yeye directly badi itakua inamhusu Ndugu yake au mtoto wake au hata rafiki yake, na kama itakua hana hao wote basi hata ya kusikia atakua nayo.

    Coach Evarist ni mmoja ya watu ambao wamesaidia kwa kiasi kikubwa mno vijana wa miaka ya 2000 kuwa na HESHIMA ya maisha, Heshima ya kazi na miili yao, kama umepita kwenye mikono yake basi utakua unajua hilo. Na kama ule usemi wa Kiswahili unaosema ‘majuto ni mjukuu’ basi ndo faida za yale alotufundisha sisi tunayaona. Tunayaona baada ya kukua maana wakati anatufundisha heshima ya muda na drills ngumu za basketball tulikua tunaona anatuonea sana sana. Binafsi nilikua naona hivyo, nilikua naona kama hanipendi maana kila mara yuko kwenye shingo yangu kuniambia lipi sijafanya vizuri. Sasa hivi nikikaa na kujiuliza kipi hasa kilinifanya nihame Pazi na kwenda kucheza basketball yangu Don Bosco ukiachana na kwamba rafiki zangu wengi walikua kule sasa ndo jibu linakuja kwamba Coach Evarist naye alichangia kwa kiasi kikubwa mimi kuamua hilo. Alikua kijana, mwenye kuujua mchezo na Don Bosco Queens ilikua ni moja ya team BORA zaidi za wasichana kuwahi kutokea miaka hiyo. Wengi wao nilikua aidha nimesoma nao Makongo au nimeenda nao Umiseta mara kadhaa kwahiyo maamuzi yangu hayakua ya kuwaza sana ingawa Pazi ndo ilikua nyumbani kwetu na itaendelea kuwa hivyo.

    Coach Evarist pia ashawahi kukutana na mitihani kadhaa mikubwa katika maisha yake, ingawa wa yeye kupata ajali mbaya ya gari mwanzoni mwa miaka ya 2000 itaendelea kusimama kuwa mtihani mkubwa zaidi ambao amewahi kukabiliana nao, ukiachana na fainali tele ambazo yeye kama mchezaji au kocha ambazo zilikua dhidi ya timu ngumu na akawahi kushinda, huu ulikua wa aina tofauti sana. Alikua peke yake usiku wa manane wakati anaenda zake nyumbani baada ya kumaliza majukumu yake aliyojiongezea ya basketball ndo mtihani huo ulipomkuta, Coach Evarist anakumbuka idadi ya watu ambao walimzunguka na kumpiga vibaya baada ya ajali hiyo. Mungu pekee ndo anajua alimuokoa okoa vipi katika lile na kwenye operesheni zake zaidi ya kumi na tano ambazo amezifanya mpaka sasa hivi zinamfanya aishi na kwanini haya yote yametokea.

    Coach Evarist ni muaminifu na mwingi wa imani, mpaka leo hii anaendelea kuishi maisha yake kama hakuna ambalo limemtokea na kubadilisha maisha na muonekano wake kwa maisha yake yote. Yule ambaye anakua na moyo kama ambao Coach Evarist anao pekee ndiye anayeweza kuishi kama ambavyo yeye anaishi. Ndo maana yeye ni wa kipekee sana.

    Yangu matumaini maongezi yetu juu ya heshima na mustakabali wa mpira wetu wa kikapu na heshima juu ya mambo kadhaa yatakuvutia na kukufunza kitu. Yangu matumaini pia uta enjoy.

    Love,

    Salama.

    1 hr 20 min
  • SE7EP13 - SALAMA NA MARDHIYA | HIARI…

    Salum Mardhiya ni mmoja ya watu maarufu sana kwenye visiwa vya marashi ya karafuu yaani kule kwetu Zanzibar. Ni mmoja ya waalimu hodari anayeongoza kwa kutoa Da’wa kwa watu ambao wanasumbuliwa na matatizo mbali mbali. Kwenye nyumba karibu zote wanamfahamu maana huonekana mara kwa mara kwenye maeneo mbali mbali ili kusaidia wale ambao wanahitaji kisomo chake. Binafsi nilifahamiana nae kupitia rafiki ambae alinitambulisha kwake mapema mwaka huu, tena haikua imepangwa wala, alikuja sehemu ambayo mie nilikuwepo kuja kupata chai na mimi bahati nzuri nilikua maeneo hayo so mtu akatutambulisha, na akaambiwa kama Mama yangu ni mgonjwa yuko hospitali na yeye akasema basi atakuja baadae kwaajili ya kumuombea dua, na jioni akatokea. Oh kama angependa kujua hali ya Mama yangu Alhamdulillah yuko vizuri. Tunamshkuru Mungu.

    Kwa mujibu wa story za hapa na pale niliambiwa nilikua na bahati sana kumpata maana ratiba yake ya kutoa Da’wa ni tight sana na watu ni wengi wanaohitaji huduma zake ila muda anakua hautoshi wa kumtilia Dua kila mtu ingawa angependa kufanya hivyo, kwahiyo ilikua kama bahati sisi kukutana na kuanzia hapo tukaanza kuwa tunaonana kwa kiasi. Nikaona si vibaya kama nitamleta kwenye meza yetu ili na sisi tuweze kumfahamu zaidi. Wakati namuambia kuhusu mualiko wa kuja kwenye kiti chetu chakavu hakua na hiyana, aliangalia ratiba yake na akaniambia hiyo tarehe atakuwepo nchini.

    Sheikh Mardhiya yeye huwa anasafiri sana, Da’wa zake huzitoa sehemu tofauti tofauti duniani, mara nyingi anakua zake Arabuni, mitaa ya Oman na Dubai na Abu Dhabi huwepo sana, kashatibu watu wa aina tele kwenye maisha yake. Kuanzia marajiri mpaka maskini, ambao walikua na imani na anachofanya na ambao hawakua na imani nae. Simu yake huita mara kwa mara na hiyo ni moja ya sababu za yeye kuwa na namba zaidi ya moja na kuwa na wasaidizi kadhaa.

    So huku kwenye kutoa Da’wa alifikaje? Hii ilikua ndo mwanzo wa maongezi yetu haya. Akiwa kama kijana ambaye angeweza pengine kufanya kazi ya aina yoyote na kujipatia rizki yake, kwanini alichagua hii? Kaniambia tokea akiwa na umri wa miaka sita, alianza kupata upeo huo, bila hata yeye mwenyewe kujua ni nini hasa kilikua kinaendelea katika maisha yake, anakumbuka pia jinsi alivyokua anazimia na kupata uwezo wa kuwasomea walokua wanahitaji kisomo chake na wanakua poa kabisa, anasema hata hakumbuki alikua anawasomea nini baadhi yao ila sasa baada ya kuwa mtu mzima na kupata kuijua vizuri Quran Tukufu ndo anang’amua nini alikua anawasomea watu ule.

    Mwanzo nilisema Mardhiya ni kijana kwahiyo kwa kiasi kikubwa ana style ya maisha ambayo vijana wengi wangependa kuwa nayo ila uwezo nayo hawana. Kama kuwa na maisha ya kifahari, magari mazuri na mke zaidi ya mmoja, pesa nyingi na nyumba nzuri zaidi ya moja na kusafiri mara kwa mara. Hii kwa ki aina flani imekua ikileta maneno na maswali kuhusu uhalali wa ambacho anafanya au ambacho amekua akifanya. Je maneno hayo yanamzui yeye kufanya ambacho anafanya kwa watu wenye uhitaji? Au kubadilisha aina ya maisha ambayo anaishi?

    Tumeongea kuhusu masuala ya Husda na wivu, usafi na mmoja kuamua kujipenda zaidi. Je kuna makosa kwenye baadhi ya matamanio ya nafsi zetu? Vipi kuhusu Sadaka? Inatakiwa itolewe ki namna gani? Ipi ni sawa na ipi si sawa? Ipi ni dhambi na ipi ni nzuri ili kuweza kuwafanya na wengine watamani kutoa? Vipi kuhusu Heshima kwa kila mmoja? Wazazi? Nafasi ya Wanawake? Kuhusu imani na uchawi kwa ambacho yeye anafanya? Mmoja anaweza kujuaje kama hii ni kufuru na hii ni sawa?

    Maswali yalikua mengi na majibu pia yalikua yanatoka kutokana na swali lilivyo ulizwa, yangu matumaini elimu ambayo Mimi nimeipata na kwako itakua vivyo hivyo.

    Tafadhali Enjoy,

    Love,

    Salama.

    51 min
  • SE7EP12- SALAMA NA DR TULIA | BULYAGA 1976

    Tulia Ackson ni jina kubwa kati ya majina makubwa kwenye Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania na kwa sisi kuweza kulipata jina kubwa na kukubali kuja kuketi kwenye kiti chetu chakavu ilikua ni BARAKA sana. Ila ukiachana na kwamba ni jina kubwa ila yeye ni binadamu, tena wa kawaida tu. Ni Mama, ni mke, ni Dada, ni Binti kwa Mama yake na ni Mbunge kwa wana Mbeya mjini lakini pia ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wadhifa ambao baada ya uchaguzi wa 2020 alirudi bungeni kama Naibu Spika ila baada ya aliyekua Spika kujiuzulu Dr Tulia aliona fursa ya yeye kuvaa viatu hivyo na wabunge nao walimpa kura zao zote za kuridhia Mwana Dada huyu AWAONGOZE.

    Baada ya uchaguzi wa 2020 na yeye alirudi bungeni kama MBUNGE kamili, si tunakumbuka baada ya 2015 alienda bungeni kama Mbunge wa kuteuliwa ila mwaka 2020 aliamua kwenda kugombea jimbo la Mbeya mjini ambako Gwiji wa Bongo Flava Kaka yangu Joseph Mbilinyi aka Sugu alikua ndo Mbunge wake? Sugu alikaa kule kwa miaka 10 ilikua ni moja ya ngome za wapinzani ambazo walikua wanajivunia nazo, kwa Dr Tulia kuamua kwenda kugombea pale iliwafanya watu wengi watake kufuatilia mchuano huo mkali ambao mwisho wa siku Dr Tulia aliibuka kidedea. Na haya yalikua ni moja ya maswali ambayo nilikua na hamu ya kumuuliza na kwa urefu alinijibu tu vizuri sana.

    Sasa nchi yetu inaongozwa na Rais mwanamke kwa mara ya KWANZA toka tulipopata uhuru wetu mwaka 1961, na hii haikuja kwa kupangwa ila baada ya kutokea ambalo Mwenyezi alikua ameliandika, na hata hili la kuwa na Spika Mwanamke (ingawa huko nyuma Mama Anne Makinda alishawahi kuwa) nalo halikua limepangwa maana Spika tayari tulikua naye baada ya Uchaguzi wa 2020. So suala la kuwa na Rais mwanamke na Spika mwanamke bila ya shaka linalipa Taifa letu utofauti na HESHIMA flani hivi ambao mataifa mengi yanavutiwa nayo.

    So kwake yeye nini hasa kimebadilika? Yaani kutoka kuwa Naibu mpaka sasa Spika? Ilikua easy kwake kuichukua nafasi hiyo baada ya kuwepo na nafasi hiyo? Alifikiria mara mbili?

    Kwa maongezi yetu haya pia nimegundua Dr Tulia alikua hapendi kabisa siasa, yeye aliyapenda zaidi maisha yake ya kuwa Lecturer pale Chuo Kikuu, alipenda zaidi kuandika na kusoma na kujifunza. Alikua akiwaona wana Siasa kama watu flani ambao pengine wanajiona tofauti na watu wengine, pengine wanajiona wa MUHIMU sana. Je na yeye sasa? Akiwa nao kule bungeni wanaishi vipi? Sasa pia kama Kiongozi wa mhimili huo wa NCHI nini zaidi kimebadilika? Nini zaidi kigumu?

    Maongezi yetu yalianzia nyuma kiasi na mbele pia yakafika, pia humu tumeongelea Tulia Trust na vitu ambavyo inafanya ili kuwafikia wale ambao wana uhitaji. Na sasa amekua naye MWANASIASA, nini kimebadilika? Msemo wa Siasa ni mchezo mchafu, kwake yeye una maana gani?

    Yangu matumaini uta enjoy na kujifunza jambo kutoka kwa Kiongozi huyu ambaye pia ni Dada yetu.

    Love,

    Salama.

    52 min
  • SE7EP11 - SALAMA NA MARTIN KADINDA | PLEASANT

    Martin Kadinda ni rafiki yangu, ni moja ya wale wana ambao hana makuu na zaidi yeye anapeeenda sana kucheka, hata ukiangalia picha zake yeye ana tabasamu tu. Pengine hiyo ndo siri ya mafanikio yake tofauti yake na wengine na pengine hiyo ndo sababu ya mimi kumpenda sana. Pia ni FUNDI, tena mzuri tu sana. Kati ya mafundi wachache WAKWELI wa nchi hii Martin ni mmoja wapo, kama hawezi hawezi, hata siku moja hawezi chukua kazi yako alafu siku ya siku akakuharibia shughuli au mtoko. Kama yuko busy na mambo yake atakuambia rafiki, hiyo sitoweza tafadhali mtafute mtu mwengine aifanye. Napenda jinsi alivyo honest maana mimi huamini sana kwenye ukweli mgumu kuliko uongo mtamu.

    Urafiki wetu ni wa miaka zaidi ya kumi sasa, anakua namuona na bila ya shaka nae ananiona nami ninavyokua, na wote tunaona kustawi kwa kila mmoja wetu, maendeleo kati yetu, challenges na urafiki wa mashaka kwa baadhi ya watu tunao wafahamu pamoja na kung’amua mambo mbali mbali kwa pamoja. Sisi si wana ambao tunazungumza DAILY ila ni wana ambao kila tulikutana basi huanzia pale tulipo ishia mara ya mwisho tulipo kutana. Hatuna neno kati yetu na wala urafiki wetu si wa KULAZIMISHA.

    Napenda jinsi ambavyo anasogea kwenye maisha yake, Martin ni mmoja ya watu wachache ambao nawafahamu ambao HAWANA HARAKA ya MAFANIKIO, HANA MASHINDANO na MTU, anafanya yake kwa SPIDI yake na anashindana na yule Martin wa mwaka jana ambaye alimuambia mwaka huu In Shaa Allah atakua kapiga hatua hii na hii na hii na kuhakikisha ile mipango na malengo YANATIMIA kwa usimamizi wa Maulana.

    Martin anawajua watu tele kwenye industries tofauti hapa kwetu na wala hutakaa umsikia akirusha majina ya watu hao ili aweze kujiingiza kwenye mazungumzo ambayo hayamhusu au hayana faida na yeye. Mara zote huwa ana focus na yale ambayo yanamhusu na wakati mwengine hayo pia ambayo yanamhusu akiona hayana muelekeo au hasara ni nyingi kuliko faida basi pia si mtu wa kung’ang’ania jambo kwasababu tu ni la mtu fulani au lina line fulani, anaamini kwenye kuanza upya na kwamba kila siku mpya ni sababu nyengine ya kuwa bora kuliko jana na ni nafasi nyengine ya kuweza kutimiza ndoto fulani.

    Baba wa mtoto mmoja ambaye alimpata akiwa mdogo tu, Martin anampa mwanawe uhuru wa kuwa mtoto na kuwa yeye na si kumtanguliza mbele kwenye maisha ya yeye kama Baba yake na kumyima uhuru wa kuishi maisha yake kama mtoto na HURU. Tushaona mifano tele hai ya ma celebrity wa Bongo ambao wanawaweka au waliwaweka watoto wao mbele na badala yake wakaishia kuwa target ya matusi kutoka kwa walimwengu na mwisho wake wazazi waishia kulalamika kujumuishwa kwa watoto wao kwenye maisha yao. Tunatakiwa kuamini kwenye kila mtu kujichagulia maisha yake ambayo anataka kuishi na hatusemi kumpost mtoto kwenye mtandao ni jambo baya sana, ila kwa jamii ambayo kumtukana mtoto na wazazi wake haioni kitu cha hatari au kuumiza au kushangaza, nadhani kwa mzazi kumuacha mtoto awe mtoto mpaka pale atakapo jitambua na kuchagua mwenyewe pengine huo ndo ungekua uamuzi sahihi zaidi. Na sisemi pia kama ni sawa kwa walimwengu kufanya hivyo, ila ukishaona kuna mwanya wa jambo kama hilo, mmoja kuamua kuchagua faragha ni jambo jema zaidi.

    Hii haikua mara ya kwanza mimi na Martin kukaa chini na kuongea kwenye TV ingawa mara ya mwisho inawezekana ikawa ni miaka 6 au 7 iliyopita lakini bado kulikua na haja na kiu ya kufanya hii, kama nilivyo kuambia hapo juu, tulikutana haijalishi ni muda gani umepita, siku zote tutaanzia pale tulipo ishia.

    Yangu matumaini simulizi za urafiki, biashara, wazazi, mtoto, kazi na kuhangaika na kuji panga na kujipa nafasi ambako kumeongelewa humu kutakusaidia kwa kiasi flani kukutoa sehemu moja na kukupeleka sehemu nyengine. Na yangu matumaini pia uta enjoy.

    Love,

    Salama.

    1 hr 3 min
  • SE7EP10 - SALAMA NA DR CHENI | SUKA

    Growing up kwenye mitaa ya Dar es Salaam na TV stations kali wakati huo zilikua na presenters makini na vijana ambao kwa kiasi kikubwa waliifanya tasnia hiyo ipendeze sana. Kuanzia vipindi vya watoto, vya muziki, filamu kutoka nje na tamthilia kutoka nje pia zilikua tamu sana, ukianza kuangalia TV kuanzia jioni hakuna mtu alikua anabanduka mpaka saa nne au tano za usiku, na kama ulikua jobless kama mimi enzi hizo basi ulikua unaunganisha na kuangalia marudio ya vipindi vya muziki ambavyo tayari ulikua ushaviona jioni yake, ila kwasababu ya utamu wake na ku enjoy kile unaona kurudia ilikua easy tu. Sasa likaja wimbi la tamthilia za NDANI, kutoka hapa hapa nyumbani, na nikiwa kama mkazi na mtoto wa Magomeni (Mtaa wa Korongo namba 10 pale kama Downing Street) 🤣 ilikua ma star hawa tunawaona tu kwa mbali na kuwaangalia kwa admiration ya hali ya juu. Cheni, au niseme Dr Cheni naye alikua ni moja ya hao watu, ah, yale ndo yalikua maisha sasa.

    Yoyote ambaye alikua anapata nafasi ya kuonekana kwenye TV alikua ananyooosha kweli kweli, chochote ambacho anaambiwa ‘acheze’ alikua anakipa uhalisia wa 100%, watu walikua na kiu ya mafanikio sana na jengine kubwa kuliko yote, watu WALIKUA WANAPENDA ambacho WANAFANYA. Na hii simaanishi kumvunjia heshima yoyote yule ambaye anaifanya kazi hiyo leo hii, ila nasemea miaka hiyo ambayo ili uweze kutoboa ilikua inabidi upate ‘upenyo’ ambao nao ukipatikana inabidi uutendee haki sana sana vyenginevyo atatokea mtu huko anakotoka ajipitishe tu kwa miondoko ya ambayo alipita nayo Dr Cheni na kupata nafasi ambayo mpaka leo ndo imefikisha hapo alipo. Again, si kwa ubaya, skuizi unaweza kuwa star wa kwenye social media tu na mambo yako yakakuendea na baada ya mwezi au wiki kadhaa kama huna jipya watu wanakusahau.

    Dr Cheni anakumbuka kama ilikua jana jinsi ambavyo alipata shavu lake la kwanza la kuwa kwenye mchezo wa kuigiza wa TV, haikua imepangwa na wenye mchezo wao ila yeye alikua amejipanga vizuri tu, alikua amenuia kabisa kwamba vile ndivyo atakavyo fanya ili aonekane na boy alionekana. Kama mtu ambaye tayari alishaanza kushika hela kutokana na kazi zake za udereva, Dr Cheni anakumbuka jinsi ambavyo alianza kuzichanga zile ambazo alikua anazipata kidogo kidogo ili atimize ndoto yake, khadithi yake kwa kiasi flani ilianzia hapo, nami nilitaka kujua hiyo heshima yake na pesa aliitoa wapi? Kutoka kuwa dereva wa daladala mpaka kuwa mmliki wa gari. Huko alifikaje? Na jibu lilikua moja tu, HESHIMA kwa PESA na HESHIMA kwa NDOTO na MALENGO yake. Alifanikiwa sana mwenzetu. Na ndo huyu mpaka leo ambaye bado anaendea kuwepo na upepo kuuhamishia kwenye ku host harusi za watu mbali mbali ambao wengi wao humpa kazi kwasababu tu walishawahi kumuona kwenye TV wakati wanakua, ukiachana na ukweli kwamba yeye ni mmoja kati ya ma MC HODARI kabisa ambao wako sasa kwenye industry hiyo.

    Akiwa kama Baba mwenye jukumu kubwa la kuiangalia familia yake inavyokua, Dr Cheni anajua kutimiza majukumu na wajibu wake wa kila siku, kupangilia mambo yake ili asiwakwaze wengine ambao wanamtegemea (hasa wale ambao anawafanyia kazi zao za harusi). Kwake yeye kuwa kwenye wakati muafaka ni kila kitu. Na hiyo kwa kiasi kikubwa imesababisha yeye kuwa chaguo la kwanza kwa wengi ambao wanataka sherehe zao zifane.

    Na je vipi sasa kwenye suala zima la filamu na maigizo? Huko nako kashakimbia? Soko limekaaje? Mipango yake ya baadae je? Yote haya na zaidi yako kwenye lisaa limoja na na dakika 16 ya Podcast hii kama utaskiliza au lisaa limoja la kuangalia naamini litakufungulia mengi.

    Tafadhali Enjoy.

    Love,

    Salama.

    1 hr 16 min
  • SE7EP09 - SALAMA NA DAMIAN SOUL | HARIRI…

    Damian Soul ni Superstar na siku ambayo sote tutakubaliana na hiyo statement basi tutaanza kufaidi matunda ya kipaji chake kwa uzuri sana, ila mpaka siku hiyo ifike ni wachache tu ambao wanamuelewa kwa upana huo ndio ambao wataendelea kufaidi kipaji chake kwa nafasi yao. Wale watu wa makampunj mbali mbali kwa mfano CocaCola ambao wanakua na events zao za ndani kwaajili ya watu wao na waalikwa wawili watatu huwa wanamfaidi sana kijana huyu hodari wa ki Tanzania. Na Damian kwa ukali wake akipata nafasi kama hiyo huwa hafanyi makosa hata kidogo, huhakikisha anapeleka mziki wote kwao ili wakati mwengine wanapokua na event basi jina lake liwe la kwanza kwenye list ya waburudishaji wao.

    Mzaliwa wa Dar es Salaam, mtoto wa Sinza kabisa, Damian amezaliwa kwenye familia ya kishua kabisa, jinsi ambavyo unaona anavaa ki nadhifu vile ukiachana na hereni zake, hivyo ndivyo Marehemu Mzee wake alivyokua ananyuka, nadhifu kabisa. Koti imenyooka na ilivaliwa inakaa hasa mahala pake, kiatu inang’aa vizuri baada ya kuipiga kiwi mwenyewe, Damian anakumbuka unadhifu huo na ki uhakika ameurithi na kuuendeleza.
    Shule kwake ilikua ni kitu tu ambacho ilibidi akifanye kwasababu pengine kila mtu au mtoto kwa matakwa ya wazazi ilibidi afanye hivyo na ili aweze kutoka pale alipokua ilibidi afunge mabegi yake mpaka Kampala nchini Uganda, kama utakumbuka vizuri kuna miaka ya kati ya 2000 hapo ilikua kama ‘fashion’ kwa watoto wa ki Tanzania kwenda kusoma kule, kwa khadithi nyingi nilizo zisikia wengi wao walikua sio waingiaji sana class na badala yake maisha ya ku party na kujitafuta na kujielewa ndo yalikua ki hivyo zaidi. Haikua tofauti pia kwa Damian Soul, Ila yeye sio kwenye ku party ila kwenye kujitafuta na kujua kwamba muziki ndo kitu alitaka kufanya kwa maisha yake yote.
    Anakumbuka mti ambao alikua anakaa chini yake na ‘kulicharaza’ sana gitaa na kila aliyekua anapita pale habari alikua nayo.
    Upekee wake wa kuanzia sauti mpaka style yake ya mavazi ndo unaomtofautisha yeye na wengine, ukimuona tu utajua kama ni Star maana jinsi ambavyo anajibeba ni tofauti na watu wengine. Hii pia inasababisha watu kujiuliza maswali kuhusu maisha yake na vitu apendavyo kama mtoto wa kiume. Yeye kwa mujibu wa maongezi haya na mengine ambayo mimi na yeye tushawahi kuwa nayo hayamsumbui kabisa. Anajiheshimu na kujielewa na pia anajua mipaka iko wapi. Na pengine kama binadamu tunatakiwa kuwaacha watu wawe wao, especially kwasababu hayo ni maisha yao, na kwa heshima na taadhima wanajua jinsi ya kujibeba kama binadamu na zaidi kama mTanzania.
    Anakumbuka jinsi ambavyo alikua Sinza hasa baada ya Baba yake kutangulia mbele ya haki, anasema mtaani palikua pa moto sana kwa kugumbikwa na wimbi la vijana kujihusisha na vitendo vya kihuni na wizi na kujikita kwenye matumizi mazito ya madawa ya kulevya. Anasema yeye alifanikiwa kukimbilia kanisani wakati anasubiria mambo yake mengine ya shule yakae sawa. Kanisani ambako alijifunza mambo ya muziki ikiwa pamoja na kujifunza kupiga instruments, ukiachana na sauti yake ya kipekee, Damian pia ni mpiga gitaa mzuri sana na muandishi hodari pia wa ngoma zake.
    Mimi ni mmoja wa mashabiki wake na binafsi nilichukua nafasi hii ili tukae chini na tuyajenge kama familia na watu wengine pia wapate nafasi ya kumskiliza na kumuelewa vizuri. Wengi wamekua wakimhukumu kwasababu tu ya muonekano wake na kama Dada na rafiki niliona kuna umuhimu wa sisi kupata nafasi ya kukaa chini na kumfahamu kinaga ubaga. Kama binadamu wote tulivyo, kila mmoja wetu ana mitihani yake ambayo anapitia, mengine mpaka leo inaendelea na mengine ilikua tunafaulu na mengine kufeli, ila kupitia huko ndo ambako kumetufanya tuwe bora na wapya na kujifunza ni jinsi gani mmoja anaweza kutengeneza maisha yake na akawa mfano bora kwa familia na jamii ambayo imemzunguka.
    Kama mtoto kwa Mama yake na kioo cha jamii, Damian yuko humble sana na wala hana papara kwenye kuhakikisha anafika pale ambapo anapaona kuna kitu cha yeye kuweza kukaa. Mpaka sasa hayuko pabaya hata kidogo maan

    1 hr 7 min

About Salama Na

From the publisher's feed

‘Salama na’ – meaning ‘Salama and’ is a one hour Podcast chat show hosted by a re known Radio &; TV personality Salama Jabir and available on Both Video and Audio of Various Platforms. In Salama…