Hii leo jaridani tunaangazia machafuko nchini Sudan, mkutano unaomulika hatua za tabianchi barani Afrika UNEA7, na juhudi za vijana nchini Kenya za kujikwamua kiuchumi kupitia kilimo endelevu.Nchini Sudan, barani Afrika, wasiwasi mkubwa unaendelea kuhusu makumi ya maelfu ya watu wanaoaminika kuwa bado wamenaswa mjini El Fasher katika eneo la Darfur,magharibi mwa nchi lakini mashirika ya misaada ya Umoja wa Mataifa yanaamini kwamba huenda yakaruhusiwa kufika katika mji huo uliogubikwa na mapigano.Leo Dunia inapoadhimisha miaka kumi tangu Mkataba wa Paris wa mabadiliko ya Tabianchi kupitishwa, wataalamu wa masuala ya tabianchi barani Afrika wanasema maadhimisho haya ni wakati wa kupima hatua zilizofikiwa lakini pia kukabili pengo linalopanuka kati ya sera na utekelezaji wa hatua za tabianchi.Kutoka mashambani hadi kwenye majukwaa ya kidijitali, vijana wa kaunti ya Kirinyaga nchini Kenya wanaongoza enzi mpya ya kilimo kinachoendana na mabadiliko ya tabianchi. Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya Watoto UNICEF limeunga mradi wa vijana uitwao Empowering Kenyan Youth in Agribusiness and Nutrition (EKYAN) kuwawezesha vijana kwa mafunzo ya vitendo na zana muhimu ili kukuza biashara zao za kilimo, kuimarisha mifumo ya chakula ya ndani, na kujenga jamii zinazohimili mabadiliko ya tabianchi.Mwenyeji wako ni Leah Mushi, karibu!