Hii leo jaridani tunaangazia Siku ya Kimataifa ya Kuelimisha Umma kuhusu Usonji, na wakimbizi wa ndani nchini DRC. Makala inatupeleka nchini Tanzania kwa mada hiyo hiyo ya elimu kuhusu usonji, na mashinani tunakwenda Gaza.Katika kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kuelimisha Umma kuhusu Usonji (Autism) mwaka huu wa 2025, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesisitiza umuhimu wa ujumuishaji na usawa kwa watu wenye changamoto hiyo akitambua mafanikio yao pamoja na changamoto wanazokabiliana nazo duniani kote.Jimboni Kivu Kaskazini, Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, Thérèse Kavira, mwanamke shupavu aliyelazimika kukimbilia mji wa Beni baada ya waasi kuvamia kijiji chake sasa ameona nusu kwenye maisha yake kufuatia mafunzo ya kuoka mikate yaliyotolewa na ofisi ya Utafiti na Usaidizi kwa Mahusiano ya Kimataifa nchini humo pamoja na ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani DRC, MONUSCO na sasa anajikimu kimaisha.Makala leo kama tulivyokujulisha ni siku ya kimataifa ya kuelimisha umma kuhusu usonji, Assumpta Massoi anamulika jinsi shirika moja la kiraia nchini Tanzania linapigia chepuo harakati hizo.Na katika mashinani fursa ni yake Marah Hajjo, msichana mdogo kutoka Gaza huko Palestina Mashariki ya Kati ambaye anasimulia mabadiliko makubwa ya sikukuu ya Eid El Fitr ambayo mwaka huu ilighubikwa na kiza cha vifusi na mateso kutokana na mashambulizi kutoka Israeli.Mwenyeji wako ni Flora Nducha, karibu!