Hii leo jaridani katika mada kwa kina tunajikita katika mkutano CSW69 ambao umebakiza siku moja tu, kesho Machi 21 unakunja jamvi, na tunamsikia Dkt. Dorothy Gwajima, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia Tanzania, Waziri Riziki Pembe kutoka Zanzibar na Profesa Smile Dzisi, Mkugenzi wa Shirika la “I believe Global” kutoka Ghana.Kamishna Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR Filippo Grandi amesema kukata ufadhili kwa mashirika yanayotoa huduma za kibinadamu kunasababisha janga la uwajibikaji. Kupitia taarifa iliyotolewa leo Geneva, Uswisi na UNHCR, Bwana Grandi amesema kukata ufadhili kunaweka hatarini maisha ya mamilioni ya watu na madhara yake kwa watu wanaokimbia majanga, yatakuwa makubwa zaidi na yataonekana wazi ikiwemo wanawake na watoto wa kike kukosa huduma zitokanazo na kubakwa.Leo ni siku ya furaha duniani maudhui yakimulika umuhimu wa watu kusaidiana na kujaliana katika masuala mbalimbali ikiwemo chakula. Ripoti mpya ya wadau wa UN iliyozinduliwa leo imeonesha kuwa nchi yenye furaha zaidi duniani ni Finland na ya mwisho kabisa ni Afghanistani. Katika 10 bora zenye furaha hakuna hata moja ya Afrika, ilihali kwenye 10 za mwisho nchi za Afrika ni 7 ambazo ni Lesotho, Comoro, Botswana, Zimbabwe, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, Malawi na Sierra Leone.Mkutano wa 69 wa Kamisheni ya Hali ya Wanawake duniani, CSW69 ukikaribia ukingoni hapa makao makuu ya Umoja wa Mataifa tumemuuliza mshiriki Wakili Rosemary Mwaipopo kutoka Tanzania mkutano umekidhi kiu yake ya kusongesha usawa wa kijinsia?Na katika kujifunza lugha ya Kiswahili hii leo mchambuzi wetu mlumbi wa Kiswahili Joramu Nkumbi kutoka nchini Tanzania, anafafanua maana ya maneno “Ashiraf, Janabi, gayagaya, kiti cha marimba na kiti cha msaji”Mwenyeji wako ni Anold Kayanda, karibu!