Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, ametoa ujumbe mzito wa Mwaka Mpya kwa ulimwengu akisema ulimwengu uko katika njia panda, ukikabiliwa na machafuko, sintofahamu na migawanyiko mikubwa na hivyo kutoa wito kwa wanadamu kuinuka pamoja kwa ajili ya haki, ubinadamu na amani. Karibu Anold Kayanda kwa maelezo zaidi.(Taarifa ya Anold Kayanda)Katika ujumbe wake wa video uliosambazwa leo asubuhi saa za New York, Marekani, kwa ajili ya mwaka mpya wa 2026, Katibu Mkuu wa Umoja wa Maraifa anauanza ujumbe wake kwa kusema, “tunapoingia mwaka mpya, dunia iko njia panda.” Amesema dunia inakumbwa na vurugu zinazoendelea, athari kubwa za mabadiliko ya tabianchi pamoja na ukiukwaji wa kimfumo wa sheria za kimataifa hali ambayo, kwa mujibu wake, inatishia misingi inayounganisha binadamu kama familia moja ya dunia.Guterres amesema watu kote ulimwenguni wanaendelea kujiuliza iwapo viongozi wao wanasikiliza kilio cha wananchi na kama wako tayari kuchukua hatua za dhati kukabiliana na changamoto hizi.Akigeukia takwimu, Katibu Mkuu ameeleza kuwa matumizi ya kijeshi duniani yamefikia dola trilioni 2.7, ongezeko la karibu asilimia kumi kiwango ambacho ni mara kumi na tatu zaidi ya misaada yote ya maendeleo, na kinacholingana na Pato la Bidhaa za ndani la Bara zima la Afrika.Amesema ongezeko hilo linatokea wakati dunia ikishuhudia mizozo mikubwa kwa viwango ambavyo havijawahi kuonekana tangu Vita Vikuu Vya Pili Vya Dunia.Kutokana na hali hiyo, Katibu Mkuu ametoa wito kwa dunia kutumia mwanzo wa mwaka mpya kuweka vipaumbele sahihi, akisisitiza kuwa ulimwengu salama hujengwa kwa kuwekeza zaidi katika kupambana na umaskini badala ya kuwekeza katika vita.Guterres amesisitiza kuwa dunia ina rasilimali za kutosha kuinua maisha ya watu, kuponya sayari na kujenga mustakabali wa amani na haki, endapo tu zitatumika ipasavyo.Kwa mwaka 2026, amewataka viongozi wa dunia kuwa makini zaidi na kufanya uamuzi unaoweka mbele maslahi ya watu na mazingira badala ya kuendeleza mateso.Aidha, amewahimiza raia wote duniani kushiriki kikamilifu katika kujenga dunia bora, akisema mustakabali wa ubinadamu unategemea ujasiri wa pamoja wa kuchukua hatua.Katika kuhitimisha ujumbe wake, Katibu Mkuu ametoa wito wa mshikamano kwa ajili ya haki, ubinadamu na amani duniani.