Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina maalum na mada yetu inamulika maoni kuhusu miaka 80 ya Umoja wa Mataifa. Pia tunakuetea muhtasari wa habari unaofuatilia ujumbe wa viongozi katika mjadala mkuu wa UNG80.viongozi wa dunia wamekutana leo hapa kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani ikiwa ni siku ya kwanza ya Mjadala Mkuu wa 80 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, ukiambatana na vikao vya kando vya ngazi ya juu. Katika hotuba yake ya UNGA 80 Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito kwa dunia kufanya maamuzi “ni aina gani ya dunia tunataka kujenga pamoja.”Kuanza kwa UNGA maana yake idadi kubwa ya wageni, Msaidizi wa Katibu Mkuu wa UN anayeshughulikia habari na teknolojia, Bernardo Mariano, amesema wamejipanga kutoa huduma ya internet (Wi Fi) kwa watu 40,000 huku wakihakikisha hotuba za viongozi zinapeperushwa bila hitilafu za kiufundi wala kuvurugwa na mashambulizi ya mtandaoni.Na Hapo kesho Jumatano viongozi wa jumuiya ya Afya ya nchi za Afrika Mashariki, Kati na Kusini, ESCA watakutana kumulika Diplomasia ya kisayansi na afya ili kusongesha Mkataba wa Zama Zijazo. Mkurugenzi Mkuu wa ECSA Dkt. Ntuli Kapologwe ameeleza kulikoni?.Mwenyeji wako ni Flora Nducha, karibu!