Ghasia zinazoendelea kwa kasi zinawakwamisha zaidi watoto katikati ya mashambulizi ya mabomu yasiyokoma, mapigano makali, na uhaba mkubwa wa chakula, maji salama na dawa kwa zaidi ya siku 500 sasa.“Hakuna mtoto aliye salama,” anasema Catherine Russell, Mkurugenzi Mtendaji wa Shrika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF kupitia taarifa iliyotolewa na makao makuu ya shirika hilo jijini New York, Marekani leo.Taarifa hiyo pia inamnukuu Catherine Russell akisema, “ingawa athari kamili bado haijulikani kutokana na kukatika kwa mawasiliano kote nchini Sudan, inakadiriwa kuwa watoto wapatao 130,000 huko Al Fasher wako katika hatari kubwa ya kukiukwa haki zao, huku kukiripotiwa visa vya utekaji nyara, mauaji na ukataji viungo vya mwili, pamoja na ukatili wa kingono.”Pia kuna taarifa za wafanyakazi wa mashirika ya kibinadamu kukamatwa au kuuawa.UNICEF inatoa wito wa kusitishwa mara moja kwa mapigano, kuhakikisha upatikanaji salama na usiokatizwa wa misaada ya kibinadamu, ulinzi wa raia hasa watoto, na kupatiwa uhakika wa njia salama kwa familia zinazotafuta hifadhi, kwa mujibu wa sheria za kimataifa za kibinadamu. Wale wanaohusika na ukiukaji lazima wawajibishwe.Wakati huohuo, Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limethibitisha kwamba Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan imewataarifu kuwa viongozi wawili wa juu wa WFP nchini wametangazwa kuwa watu wasiotakiwa nchini Sudan na hivyo wameamriwa kuondoka nchini humo ndani ya saa 72, bila maelezo yoyote.WFP inaeleza kwamba uamuzi huu wa kuwafukuza Mkurugenzi wa WFP nchini Sudan na Mratibu wa Dharura wa WFP nchini humo unakuja katika kipindi muhimu kwani mahitaji ya kibinadamu nchini Sudan hayajawahi kuwa makubwa zaidi kama kipindi hiki, huku zaidi ya watu milioni 24 wakikabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula na jamii zikikumbwa na baa la njaa.Wakati ambapo WFP na washirika wake wanapaswa kupanua wigo wa msaada, uamuzi huu unalazimisha shirika kubadilisha uongozi bila mpango, jambo linalohatarisha shughuli zinazowaunga mkono mamilioni ya Wasudani walio hatarini kukumbwa na njaa kali, utapiamlo, na hata kifo kutokana na njaa.WFP na maafisa wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa wanaendelea kuzungumza na mamlaka za Sudan kupinga hatua hii na kutaka ufafanuzi wa uamuzi huo.Tags: Sudan, El Fasher, WFP, UNICEF