Moja ya changamoto iliyokatisha ndoto za watu wengi, ni ile ya kukataliwa ama kupingwa.
Watu wengi wamekutana na hali hii, kuna ambao wameweza kuishinda, pia kuna ambao imekuwa kikwazo kwao.
Jambo moja muhimu la kufahamu ni kwamba kukataliwa ni suala la kawaida, hata uwe bora kwa namna gani sio kila mtu atakubaliana wewe.
Watu watakukataa kwa sababu zao wenyewe, wapo ambao watakukataa kwa sababu ya hofu yao juu yako, lakini pia kwa sababu kile ulichonacho wao hawana.
Sasa unapokutana na hali hii hakuna haja ya kukata tamaa ama kupoteza muda wako kubishana nao. Kuna mambo muhimu unayopaswa kufanya;
1. Ongeza kujiamini.
Badala ya kukata tamaa kwa sababu ya kukataliwa, jambo la muhimu ni kuongeza kiwango chako cha kujiamini. Amini katika uwezo wako, amini katika kusudi lako.
2. Toa matokeo.
Ni rahisi sana mtu kubishana na maneno yako lakini ni ngumu kufanya hivyo dhidi ya vitendo vyako.
Toa matokeo katika kile unachokifanya, ikiwa watu hawaamini kama unaweza kuimba, imba ili waamini, ikiwa hawaamini kama unaweza kuandika, andika ili waamini.
3. Sikiliza sauti yako.
Badala ya kukata tamaa kwa sababu ya maneno ya watu wanaokukataa, wewe sikiliza sauti iliyoko ndani yako.
Hii ni ile sauti iliyokwambia uanze kufanya hicho unachokifanya, kamwe usijaribu kuisaliti itumie kama ngazi ya kusonga mbele. Kwa sababu sauti hii ndiyo inayokufahamu zaidi kuliko mtu mwingine yeyote.
Kumbuka, ukitaka kuacha jiulize kwanini ulianza.
Usikate tamaa kwa sababu ya kukataliwa ama kupingwa, kumbuka wewe sio wa kwanza kukataliwa na huwezi kupendwa na kila mtu hata Mungu hapendwi na wote. Hivyo jiamini na uamini ulichonacho, kisha songa mbele.
Imeandikwa Na Zakayo Iganja, Na Podcast imefanywa Na Innocent Ngaoh