Salama Na

Salama Na

Download on the App Store

Salama Na episodes

  • Ep. 43 - Salama Na MANTANA | MIPANGO BAABA

    Sniper Mantana si jina lake la Serikali na ukiskiliza kwa makini kwenye maongezi yetu haya utaelewa uzuri kwamba jina hilo alipewa kutokana na umahiri wake wa kulenga pale kwenye malengo yake na kufanikiwa kutokana na juhudi zake ambazo unaziona hata kwa mbali tu na ki ukweli kabisa hiyo ni moja ya sababu kubwa ilonifanya nitake kukaa naye chini ili anifahamishe hasa siri ya mafanikio yake na kile kinachomsukuma kufanya afanyayo.

    Mara ya kwanza kumsikia Sniper ilikua kutoka kwa AY ambae yeye walikutana huko Malaysia na alikua ni msanii wa kwanza kwenda kutoa burudani huko, Sniper ndo alifanya mipango yote hiyo. Alikua na uwezo wa kuwakusanya wanafunzi wenzake wa ki Tanzania, Kenya na Afrika kwa ujumla na hata wageni wa mziki wetu pamoja na kuwapa burudani kutoka ukanda huu. Alifanikiwa, aliweza kuwa na sehemu ya kupiga disco na concerts na aliweza kusoma na kurudi na digrii yake vizuri tu kabisa.

    Kampuni yake ya Straight Up Vibes ndo kinara sasa hapa kwetu kwa kufanya kazi nyingi za makampuni na promotion ila pia yeye kama yeye pia ni promoter aliyetulia kabisa, anayejielewa na ambeye pia amefanikiwa vizuri kuliteka soko la muziki hapa nyumbani kwa kuweza kuwaleta wasanii wa nje ambao wameweza vizuri tu kwa kutoa burudani ambayo wanastahili kwa viingilio vikubwa wanavyolipa.

    Kampuni yake ilifunga mwaka jana kwa concert ya heshima kabisa na mwaka huu ameuanza vizuri tu kwa kuendeleza pale alipoishia.

    Humu, binafsi nilitaka kujua safari yeke na mambo mengine kama haya lakini pia niliongea nae kuhusu mustakabali wa muziki wetu hapa nyumbani, kwa kirefu tu. Yeye kama promoter amekua akidondosha wasanii wengi hapa ambao wengi wao wamekua wakilipwa mapene mengi na hilo likasababisha baadhi ya wasanii na raia wa kawaida kuuliza maswali juu ya sisi kuendelea kuwatajirisha wenzetu wakati hapa nyumbani yuna vipaji vikubwa ambavyo navyo vilikua vinahitaji kupewa mapene hayo , na kama kuna sehemu wanakosea basi waambiwe ni wapi ili nao watoke! Mantana hakua mchoyo juu ya nini kinatakiwa kufanywa na pia kwamba mlango wake uno wazi kwa yoyote atakayehitaji msaada wa jinsi ya kufanya mambo kadhaa ili vitu viende.

    Sniper ni MTANZANIA, kijana aliyeenda shule na kumaliza kabisa na kupata cheti chake freshi kabisa. Hakukimbia DARASA, alifanya alichokifanya na kujifunza along the way, elimu ambayo inamfanya atoe ajira hapa nyumbani na kuishi vizuri pia. Nilimleta hapa ili yatu waskie alipotoka na nia na madhumuni yake huko mbeleni na kama vipi uchote mawili matatu ili yaweze kukusaidia hapa na pale. Tafadhali Enjoy.

    Love,

    Salama.

    1 hr 38 min
  • Ep. 42 - Salama Na EDO KUMWEMBE | MWENYE SHOKA HAKOSI KUNI

    Edward ‘Edo’ Kumwembe ni rafiki yangu wa si miaka mingi, pengine sita tu toka mara ya kwanza kukutana nae wakati wa uzinduzi wa kampuni moja ya kamari hapa nyumbani. Nakumbuka alikua akimtania sana Fid Q na jinsi ambavyo Fid alikua hamjibu Edo ndo ilikua inachekesha kabisa, wengi wetu tunafahamu Fid ana maneno mengi, ila mbele ya Edo huwa hana hata maneno kabisa. Tulicheka sana, na baada ya hapo tukaanza kufanya kazi pamoja kama Influencers kwenye hiyo kampuni, na baada ya miaka  mitatu Allah akabariki nikapata ile kazi ya Super Sport, na kama ulikua hufahamu, Edo ndo alinipigia chepuo nyingi sana ili niweze kuipata hiyo kazi ambayo kiiila ‘mchambuzi’ wa futiboli alikua anaitaka, mpaka baadhi ya wastaafu na viongozi walikua wanaitolea macho, lakini Mungu akanibariki nayo mimi Salama. Yeye pia (hii ilikua siri 😃) ndo alikua mtu wa kwanza kuniambia kama mkeka umetiki, tunaenda zetu Johannesburg. Furaha yangu ilikua kubwa sana, na nilikua napiga kelele ndani yangu, ila kwa nje nilikua na play cool, najifanya oh. okay…Habari nzuri hii Edo, asante sana. Kumbe ndani kuna Meja Kunta anaimba singeli kwenye pati ya kitaa, kelele nyingi sana.


    Mungu si Athumani na safari yangu kwa kwanza ya KIKAZI ilikua ya AFCON2018, unaweza aka guess ni nani nilipangiwa kufanya nae kazi kwenye kuanzia mechi za mtoano mpaka fainali hizo? Ndio umepatia, ni Edo Kumwembe. Alifanya maisha yangu yawe rahisi sana. Alinisaidia sana kunitoa hofu na kunifanya niwe calm na kuweza kuifanya kazi ile kwa uzuri kadri ya uwezo wangu, akiniona tu niko down au siko 100 alikua akiniambia, ‘oya, hii kama ubwabwa tu’. Huo ulikua ni msemo wa Maulid Kitenge ambao Edo aliuleta kwangu akimaanisha hii kazi ni rahisi sana, ni kama kula wali tu 😄. Mungu ni mwema. kazi ilienda freshi, Edo alinipa bata la kufa mtu. alinionyesha (na bado anaendelea) kunionyesha Jozi. Ananifundisha mambo mengi kuhusu soka na watu wake na kila kitu chake kila siku, hata kama haniambii mimi ila najifunza tu kutoka kiwale kila siku.

    So nini hasa ambacho kinamfanya Edo awe ‘mnyama’ kiasi hiki? Well, ndo Mungu alivyo mbariki. Hana kununa wala kulalamika ili mambo yawe magumu, yeye huchukulia vitu kwa wepesi tu na kumalizana navyo vizuri tu. Anafanya anachokitaka kwa wakati wake. Hana majungu, hasemi pembeni yani, kama ana la kukuambia basi jua atafanya hivyo bila ya kukupepesa, kitabia flani ambacho tunafanana kiasi. Urafiki wetu pia unaendana kwa kupenda kucheka, kama nilivyosema awali, ukikaa naye kucheka ni uhakika na hilo pia ni jambo langu pendwa kabisa. Inawezekana ikawa anakusema wewe mwenyewe mpaka inabidi ucheke tu, inawezekana ikawa kuhusu football, au siasa au muziki au maisha, mapenzi yani wewe tu. Kusema za ukweli ni raha tu ukiwa nae. Pia anapenda MAISHA MAZURI na haogopi kuyafanyia kazi ili aishi hivyo. Pia yeye ni moja wa waandishi wa habari wachache sana ambao wanajituma sana, Edo anaweza kuweka hela zake akasafiri tu ili aweze kufanya interview zake na zikawa tofauti kabisa na waandishi wengine. Hii inampa uwanja wa kufanya vizuri zaidi na kupa uhuru wa kuongea anachokijua na sio kuongea tu kutokana na alichosoma kwenye internet.

    Tulipokutana mezani tuliongea kuhusu yeye kama toto kutoka kwenye familia ambayo haikua vibaya, familia ya kisomi tunaweza kusema. Vipi alianza kufanya anachofanya sasa? Nani alimvutia? Pia kuna mustakabali wa mpira wetu hapa? Simba na Yanga? Ni kweli soka letu limepanda kiwango? Vipi kuhusu wachezaji wetu wanaocheza soka nje ya Tanzania? Chama cha mpira je? Viongozi wake? Mpango wa mbeleni anauonaje? Je, unafahamu kama Edo pia ni muandishi mzuri sana wa makala mbalimbali kwenye gazete la Mwananchi na Mwanaspoti?

    Maongezi haya yangeweza hata kufika siku ya pili maana mimi na yeye tunaweza kuongea na kucheka  for days ndo maana mimi na wenzangu tukaona sio mbaya kukuletea Kaka hapa ili nawe ufaidi na kujifunza kama ambavyo mimi nafanya. Yangu matumaini ata enjoy.

    Love,
    Salama

    1 hr 13 min
  • Ep. 41 - Salama Na KALITO | THE ORIGINATOR

    Carlos Bastos aka Kalito ni moja kati ya wale binadamu ambao hawahitaji ‘kutambulishwa’ na hiyo si kwa sababu ya muonekano wake hata kidogo zaidi ni personality yake, anaongea, anachekesha, anajielewa, anajua nini cha kusema na wapi pa kusema pia. Katika watu ambao namshukuru Mungu kwa kuwafanya wawe rafiki zangu Kalito ni mmoja wapo.


    Jinsi ambavyo alifika Tanzania inaweza ikakufanya ujue pia yeye ni mtu wa aina gani haswa, kutoka mwenyewe familia ambayo mtoto wa kiume ni pekee, na pengine alikua na uhakika wa kupata kila anachotaka lakini aliamua kupaki begi na kuchanja mbuga kuja hapa Tanzania. Kusema za ukweli story yake ya maisha ni ya kuamsha sana. Imagine wewe leo unatoka ulikotoka ukaenda zako pa kwenda, ukajimix kwa kuhudumia watu kwa kuwapa burudani na chakula mpaka akapata upenyo wa kufanya yake. Ni wangapi kati yetu wanaweza kufanya hivyo? Najua wengi wetu hatukuzaliwa hapa Dar es Salaam ila tumekuja tukalikita na mpaka sasa Alhamdulillah mambo yanaenda. Ila si wengi wanaweza kusema hivyo. Tunajua huchukua jasho machozi na pengine damu kufikia malengo.

    So binafsi haswa nimejifunza au najifunza nini kutoka kwa rafiki yangu huyu kila siku? Cha kwanza ni kuwa MKWELI. Kama unayo unayo, kama unaweza kufanya/kufika utafanya hivyo, kama unaweza kutoa unatoa na kama huwezi UNASEMA. Naamini ndani ya moyo wangu, hiyo ni moja ya silaha kubwa sana kama unataka kufanikiwa, kama unataka MAENDELEO. Cha pili pia ambacho bado kinakaa kwenye UKWELI ni UAMINIFU. Ukikopa pesa RUDISHA maana hii itakupa nafasi ya kuweza kurudi na kukopa tena kama mambo yako yatakua bado sio sukari, sasa imagine hujarudisha na ukapata shida nyengine je utaweza kurudi kukopa tena? Vipi kama alokukopesha nae kashawaambia ma don wenzake kwamba wewe huwa hulipi? Utasogea kweli?... Mwisho wa siku DAWA YA DENI ni KULIPA tu.

    Jengine KUBWA zaidi ni kutokua na SIRI nyiiiingi. Mambo ambayo yatakufanya uwe unaweka vitu vingi ndani, ambavyo hauwezi kusema labda kwasababu ya aibu au pengine hauko huru kuviongea nalo ni TATIZO. Ni kweli sote tuna SIRI zetu, ila zikizidi ndo zinaleta msongo wa mawazo. So kuwa muangalifu na kipi unasema na kipi unaweka. Kujijazia mavitu moyoni ki afya si mpango hata kidogo.

    Kalito yuko HURU, anaskiliza watu na kujifunza kila siku pia kama mimi na wewe tu, pia ana shida zake ambazo kwa kiasi kikubwa ameweza kuzifanya zisiwe chanzo cha yeye kutokua na furaha au kumpa unyonge. Pengine unaweza kusema ni kwa sababu ana hela au biashara inayomuingizia kipato kila siku ndo maana ni rahisi kwake kucheka kwa yote, ila Amini nikikuambia hata yeye huwa ana kutana na mitihani mikubwa tu, lakini kwasababu yuko POSITIVE muda wote unakuta anamalizana na shida zake kwa roho safi tu. Anakubali pale anapokua kashindwa na kujifunza na anafurahia pia challenges ambazo binafsi anazishinda kwa uzuri tu. Yeye pia ni rafiki nambari MOJA wa wafanyakazi wake karibia WOTE wa Samaki Samaki na sasa Kuku Kuku wa kuwajua mmoja mmoja kwa majina yao. Mpaka mafundi wake wote hao ni familia yake.

    Wangu tumekuletea Kalito kwenye meza ili uone mambo kwa utofauti haswa. Ujifunze kutoka kwa watu ambao unawaangalia kila siku na ambao pengine unadhani mambo yao ni SUKARI kila siku iendayo kwa Mungu. Yangu matumaini utaokota mawili matatu humu. Maana ukiachana na biashara pia alizungumza maisha yake. Alivyoumwa, watoto wake na jinsi alivyofika Tanzania na nchi yetu hii na watu wake. Alituambia pia kuhusu mapenzi yake na Bahari na mahusiano yake na watoto wake na Mama yao ambaye hayuko nae tena sasa. Tafadhali enjoy.

    Love,
    Salama.

    1 hr 20 min
  • Ep. 40 - Salama Na KADUGUDA | SIMBA WA YUDA

    Mara ya kwanza kukutana na Mwina Kaduguda na tukaongea kiasi ilikua kwenye seminar ambayo timu ya Simba ya wanawake ilikua imeandaliwa kwaajili ya kuwaweka sawa kwenye masuala ya biashara, jinsi ya kujitunza wao na vipaji vyao, jinsi ya kuishi na umaarufu na pia kusimamia masuala yao ya kifedha. Mzee Kaduguda alikuwepo kwenye kikao hiko akiwa kama Mwenyekiti wa klabu ya Simba, na pia mmoja wa watoa nasaha kwa mabinti hao.


    Na kusema za ukweli toka siku hiyo baada ya kumsikiliza akiongea na wachezaji wale pamoja na Mimi ambaye nilikua mgeni tu kwenye seminar ile, nilivutiwa sana na nikasema haitakua vibaya hata kidogo kama nikipata wasaa wa kuzungumza na mtaalam huyu wa Siasa za kambumbu la Tanzania na Afrika kwa ujumla, mwamba ulojaa uerevu wa kusoma kuhusu soka letu lakini zaidi historia ya Simba Sports Club na zahma za hapa na pale pamoja na siku za neema zaidi ambazo zimeshawahi kutokea pale Msimbazi, mtu pekee anayeweza kukukhadithia yote hayo ni Mwina Mohamed Seif Kaduguda.

    Toka siku ya kwanza alipomuambia Mama yake mzazi ndoto zake na ambae pia alicheka sana, Mwina hakuwahi kurudi nyuma asilan, badala yake alisoma kwa bidii mno mpaka siku alipofika chuo kikuu. Na baada ya hapo pia hakuacha kujiendeleza, aliendelea kwa kusomea leseni kwa kufundisha mpira na hapo ni baada ya kuwa mmoja wa waandishi wa habari za michezo waliobobea kabisa. Alitaka kuwa tofauti na bora kuliko waandishi wengine, na alifanikiwa vizuri tu.

    Msukumo huo sasa unatoka wapi? Na pale Simba Sports Club aliingiaje? Lini ndo alijua ana mapenzi na club hii na si nyengine? Kuna mtu alikua anamvutia? Alimshawishi? Alishawahi kuichezea? Alishawahi kuwa footballer yeye? Vipi uongozi alifikaje huko? Na ramani ya soka letu je anayo nani? Inasomeka? Kuna kitabu cha historia ya Simba SC toka miaka ya mwanzo kabisa yeye ndo aliandika, je nini kilimpa msukumo? Inasemekana ndo kitabu ambacho kimefanyia research na kuandikwa vizuri zaidi, je kuna ukweli ndani yake? Na kwamba kinauzwa bila ya yeye kupata malipo yoyote?

    Akiwa kama Mwenyekii wa SSC yeye haswa jukumu lake ni nini? Kuna ukweli wa hizi habari kuhusu tajiri kutoweka hela alizo ahidi? Yeye kama Kiongozi hili analizungumziaje? Mipango kwenda mbele ikoje? Na vipi kuhusu uhusiano wake na Mo Dewji? Na maamuzi ya kuwa CEO wa klabu ni MWANAMKE hayo vipi? Na je alishirikishwa kwenye maamuzi hayo?

    Enjoy mazungumzo yangu haya na Simba, ingawa alikua mzungukaji kweli kwenye ujibuji wa maswali yangu niseme tu nimemuelewa. Hakuna kitu kinajengwa ki rahisi au kwa siku moja. Simba Kama klabu inabidi ipewe muda na mipango thabiti ili kufika kwenye malengo makuu na Ndugu Mwenyekiti hilo analitambua.

    Regards,
    Salama.

    1 hr 16 min
  • Ep. 39 - Salama Na DULLA | GO HARD OR GO HOME...

    Abdallah Khamis Ambua ndo jina halisi toka kwa wazazi wake ambao hawana asili ya kisiwani wala kuwahi kuishi huko kwa muda mrefu ambako pengine ndo kukamuwezesha kupata hiyo lafdhi. Kabla hatujafika kokote kwa kuskia kutoka kwangu, ningepeda ufahamu kwamba mimi si mmoja ya watu walotaka Dulla apewe kipindi cha Planet Bongo mwaka 2018 wakati naenda zangu Cardiff kushangaa kondoo, na moja ya sababu zangu kubwa ilikua yeye kutokua na lafdhi nzuri ya maneno kwenye lugha yetu adhimu ya Kiswahili. Na hilo nililiweka wazi haswa. Lakini pia nilikubaliana na matokeo baada ya viongozi kuamua kumpitisha yeye, na kwa heshima zote leo napenda kuchukua nafasi hii kuwapongeza kwa kazi nzuri waliyoifanya, kwa kuona kijana ambaye alikua na utayari kwa kujifunza, wa kujua kwamba alikua hajakamilika na mlango ukawa wazi kwake kutaka kujifunza na kuwa bora.


    Tupeleke miaka mbele mpaka 2020, ingawa hapo nyuma tushakutana mara kadhaa na nikamuambia jinsi ambavyo ananifurahisha kwa kukuwa kwake na kwamba mimi ni mmoja wa watu wanao jivunia yeye. Na hata wakati tunafanya maongezi yetu haya, nilimfahamisha pia. Mwanzo wakati naanza kuandika nilianza kwa kukuambia kuhusu asili yake, sababu ilikua ni juu ya lafdhi yake ya kimwambao ilonyooka haswa. Mimi wakati nakutana na Dulla kwa mara ya kwanza kwenye usaili hakua na hiyo accent, alikua na matatizo ya R na L na pia hakua ‘original’, alikua ana tangaza na kuongea kama B Dozen, ambaye tayari alikua amesha ji establish vizuri tu na anga yote alikua anaunguruma yeye mara ifikapo saa nane kamili ya mchana. So kama mtangazaji mpya anayechipukia, Dulla hakua na nafasi ya kuweza kutamba mbele ya Dozen, na wala hakua na uwezo wa hata robo yake. Kwa yeye kutoboa na kuweka alama yake ilikua inambidi awe YEYE na aje na ladha YAKE.

    Leo hii, mimi na enjoy haswa ninapomsikiliza Mjukuu wa Ambua radioni, sauti tamu, matamshi yamenyooka, ladha ya maneno inatulia maskioni, hapayukwi kwenye kipaza sauti na pia kubwa kuliko yote ana akili, akili ya kusema na kuuliza maswali muafaka na muda muafaka. Na kwa hilo namheshimu.

    Basi nikataka kujua vile alijiskia alipong’amua kama mimi sikua shabiki yake hata kidogo? Na Kama ilimtoa katika ‘mchezo?’. Wakati mshindi wa mtangazaji mpya wa Planet Bongo anatangazwa tayari Mimi nilikua nishafika zangu Cardiff kwahiyo sikuwahi kuongea nae tena kuhusu uchaguzi wake na wala maendeleo yake kwahiyo hii imekua mara ya kwanza tuna discuss. Pia nilitaka kujua kuhusu mke wake, watoto, Kaka yake ambaye naye ndo alimfanya kwa kiasi kikubwa achague kazi hii anayofanya sasa. Pia kuhusu mahusiano yake na Diamond Platnumz na Ali Kiba, muziki wa Bongo Flava kwa ujumla. Kazi, mapenzi, ujana, dini na yeye kama binadamu. Haya yalikua maongezi flani ya kikubwa ambayo nimefurahi tuliyafanya mimi na mdogo wangu huyu.

    Kama kawaida, yangu matumaini hii pia itakufunza jambo, itakutaka uwe bora na kutokubali kushidwa hata kama ulokua unapenda sana akupe sapoti akawa haamini juu ya uwezo wako, hiyo ndo iwe chachu ya wewe kutaka kufanya vyema zaidi.

    Love,
    Salama

    1 hr 12 min
  • Ep. 38 - Salama Na CHARLES HILLARY | MZEE WA BUSARA

    Ilinichukua muda mrefu kuweza kupata nafasi ya kuongea uso kwa macho na Charles Hillary, maana toka enzi za Mkasi nilikua natafuta mwanya wa kuweza kukaa nae chini walau kwa hata nusu saa tu. Sikuwahi kukata tamaa badala yake nilikua kama chui kwenye mawindo yake, na mwisho wa siku kwa uwezo wa Mungu, binti yake Faith, Ivona Kamuntu na Mama kule nyumbani waliniwezesha kushinda mechi hii hatimaye. Mungu anajua tabasamu lilikua la ukubwa wa kiasi gani, na pengine hilo linaweza likawa limefanya niwe excited sana mpaka mengine nikayasahau kuyauliza, au kujua naulizaje, au kushangaa sana? Ushawahi kukutana na mtu alafu ukasahau yote ulotaka kuyasema, au kufanya. Ukabaki tu umeganda kama sanamu? Bado? Basi we ngoja tu.

    Simkumbuki Charles Hillary wa Radio Tanzania (RTD), namkumbuka wa Radio One zaidi. Wa taarifa ya habari, wa kipindi cha charanga, wa kutangaza mpira, huyo ndo ambaye alinifanya mimi nipende Radio, nipende kuskiliza mpira na pengine kuutangaza. Sauti yake tamu na lafdhi ilonyooka ilikua inakufanya uone kama unaona haswa anachokiongea. Kipaji cha kipekee kabisa. Kipaji kutoka kwa Mwenyezi Mungu ambacho pia kilihitaji kujituma na kujitetea na kujiamini sana. Kutimiza ndoto si suala la kulala na kuamka tu, suala la kukosa usingizi. Suala la kutokwa na jasho, suala la kulia kwasababu tu unadhani hakuna anaye skiliza mawazo yako na ndoto zako... Mpango ni kutokata tamaa kamwe! Hayo ni baadhi tu ya mambo ambayo yeye alipitia na akaja akawa Lejendari huyu tumpendaye na kumheshimu wote.

    So nlitaka kumfahamu zaidi, na huwezi kumfahamu mtu kama hujauliza maswali, so tulianzia kwenye asili yake na elimu, na kwa Mama yake ana Baba yake, kwenye kazi yake ya kwanza, vipindi vigumu katika maisha yake, transfer za kazi. Pia jinsi alivyokutana na Mama wa watoto wake, na zaidi tulimzungumzia Mama wa mtoto wake wa pili, wa kwanza hatukumzungumzia, skuona sababu ya kufanya hivyo maana alikua excited zaidi kumuongelea Sarah, ambaye anampikia wali na njegere zilizonyooka zaidi dunia nzima . So alikutana naye vipi? Mwaka gani? Pia tuliongea kuhusu teknolojia na jinsi ambavyo yeye anaenda na wakati. Mahusiano yake na Ivona Kamuntu na AzamTV kwa ujumla.

    Kama nilivyosema mwanzo wa story yangu hii na Charles Hillary, naomba ufahamu kwamba hii ni moja ya interview nilizokua natamani kufanya na natumai pia uta enjoy na pia utajifunza chochote kitu kwenye suala zima la utafutaji, malezi, ndoto na mipango maana binafsi nimechota kadhaa. Lejendari akija mezani unachotakiwa kufanya ni kuskiliza zaidi na kuongea kidogo.

    Enjoy.

    Love,

    Salama.

    1 hr 15 min
  • Ep. 37 - Salama Na DR MWAKA | BINGWA

    Sikuwahi kukutana na Dr Mwaka mimi kabla ya tarehe 26 ya mwezi wa tisa, ila nilishawahi kuongea nae kwa simu mara mbili kabla ya kukutana, hatukuwa marafiki ila maongezi yetu ya mara ya kwanza kwenye simu yalinifanya nijue kwa kiasi yeye ni mtu wa aina gani, na nilivyokutana nae pia iliongeza heshima yangu kwake kwa kazi anayofanya na aina ya mtu yeye alivyo. Nisiseme kwa kupepesa, alini impress na nilijifunza vitu kadhaa kwa muda mchache niliokaa naye na kuongea nae.


    Alikuja na mkewe kwenye set ya kipindi na alihakikisha mkewe anafika mpaka kwenye ‘kizuizi’ cha mwisho kabisa kabla ya kufika kwenye meza ya mahojiano na pia alihakikisha macho yake na ya mkewe yanagongana kila anakapopenda kufanya hivyo. Wakati mwengine watu hufanya mambo kwaajili ya camera ili wapate kuongelewa, ila kwa wanaopendana kila kitu huwa kinakua wazi, jinsi wanavyoongea, wanavyocheka, wanavyoangaliana na mengineyo imenipa sababu ya mimi kukubali kwamba wawili hawa ni wanapendana kweli. Na tukumbuke kwamba huyo si mke pekee wa Dr JJ Mwaka kama sote tunavyofahamu, ila hakuna ubishi kwamba yeye pia ni mke wake pendwa kabisa.

    Maongezi yetu yalianzia kwenye asili yake kama kawaida, na aina ya maisha anayoishi sasa. Kama ni kipaji au alienda shuleni kusoma haya anayoyafanya, na suala la yeye kuwa Daktari Bingwa wa nguvu za kiume na mambo ya uzazi wa kina Mama, na kama hizo tu ndo tiba yeye hufanya. Alinza lini? Alirithishwa? Na je wakati mwengine maneno watu wanasema juu yake yanamkera au yanampa motisha ya kufanya zaidi? Unaikumbuka ile skendo ya kutaka kufungiwa ofisi? Aliimalizaje? Na chimbuko lake haswa hiyo story ni wapi? Ilikuaje akachomoka humo? Na Kuna khadithi na mahusiano yake na wake zake? Hana mmoja mwenzangu. Anawezaje kukaa na wote? Alishapitia ndoa ngapi? Je kasomea taaluma yake hii? Biashara ina faida? Je kuhusu skendo ya kutumia magonjwa ya wanawake na kujipatia wake ni kweli?

    Kusema za ukweli tumeongea sana, na nimejifunza sana kupitia mazungumzo haya na kama ilivyo ada natumai na wewe utaokota mawili matatu na pengine kupata idea ya ajira na kujikwamua kwa hapa na pale. Dr Mwaka pia ni mtu anayependa watu wengine waendelee na aliniambia kama kwa yeye kuja kwenye kipindi kutasaidia hata kwa theluthi tu na kufanya vijana na wengine wajiongeze basi angependa kuja na alifanya hivyo, kwa hilo namshkuru sana. Tafadhali enjoy rafiki.

    Love,
    Salama.

    1 hr 18 min
  • Ep. 36 - Salama Na JOH MAKINI | KIUNGO

    Story ya kwanza siku zote itakua ni jinsi ambavyo mimi na Joh Makini tulipokutana mara ya kwanza, nakumbuka vizuuuri sana sana haswa, jinsi alivyokua mwembamba na asiyekua na maneno mengi, ila macho yake, macho yake yalikua kama Askari wa shabaha ambaye akilenga hawezi kukosa, na guess what?


    Wanasema katika vitu ambavyo havibadiliki kwa binadamu anapokua basi macho ni moja wapo. Macho yake ni yale yale ya sniper, ila kwa sasa ni ya sniper aliye relax ambaye shabaha zake na malengo yake yanaeleweka. Hahitaji kujitambulisha anapokua kwenye mawindo yake. Heshima zangu nyinyi zinaenda kwake, maana kuweza kukaa kwenye chati toka mwaka 2004/05 mpaka leo hii si jambo ambalo kila muwindaji anaweza kufanya.

    So anawezaje? Kipi haswa kinamsukuma mwenzetu huyu kuweza haswa kuendelea na kuwa relevant kiasi hiki? Mimi nimefahamiana naye zamani tu, hiyo miaka ya mwanzo ya 2000 na maendeleo yake na kazi yake kama nilivyosema inajielezea. So swali ni anawezaje au amewezaje? Jengine unalotakiwa kufahamu ni kwamba Mwamba si muongeaji sana. Yeye vitendo ndo zaidi. Na mashairi yake ya kibabe na style laini na nyeusi ndo inamfanya aendelee na yake. Kuweza kuweka kundi la Weusi pamoja na kuwa na discipline ya kazi nayo vipi? Kufanya kazi na mdogo wake ambae ni msomi na kama mwenye maneno mengi wakati mwengine inakuaje? Na yeye na Lord Eyes na GNako walitoana wapi? Sawa wote wametoka Arusha ila huu muungano ulikua wazo la nani? Je ki biashara inawalipa?

    Pia tuliongea kuhusu muziki wa sasa, wa ki leo na mbinu ambazo baadhi ya wasanii wanazitumia ili kufikisha ujumbe wao. Mambo yamekua kama mengi ivi, yeye mawazo yake kwenye hizo mbinu ni yepi? Ashawahi kuchanganyikiwa na baadhi ya vitu ambavyo anaviona mtandaoni? Na kama ana wivu?

    Kuhusu familia pia nlitaka kuchimbachimba kidogo lakini alikua ngumu maana Joh na familia yake huwa anakua mlinzi haswa. Ni mwaka huu ndo ilikua mara ya kwanza kuona anaweka picha za mwanawe King kwenye Instagram yake. Kwa sababu ambazo yeye anazijua ameamua kufanya hivyo, ya nyumbani ni nyumbani na ya sanaa yake ndo yanaenda mitandaoni. Hapo nilimheshimu sana kwa hilo.

    Hip Hop si muziki wa lele mama, ni aina ya muziki wa majigambo haswa na maneno tu peke yake hayakufanyi uwe bora mbele ya wana hip hop wenzako bali uwezo wa kuyatembea unayo yaongea na kukaa juu siku zote za maisha yako ndo heshima hapo inapopatokana, na naamini kwa Joh, hilo hatuna deni nae, au niseme binafsi, SIMDAI. Haya, kama ilivyo kawaida yetu yangu matumaini utapata mawili matatu hapa ya kujisogeza na maisha yako na mipango endelevu, na pengine jinsi ya kutokata tamaa katika maisha na kuamini ndani ya mipango yako na maendeleo yako ndugu yangu. Tafadhali enjoy pia.

    Love,
    Salama.

    52 min
  • Ep. 35 - Salama Na KAJALA | JERAHA LA MOYO

    Kajala Winfrida Masanja ndo jina lake alipopewa na Mama yake kipenzi alipozaliwa. Mama ambaye alikua akilitumikia jeshi la Polisi Tanzania miaka ya nyuma, ambaye alihakikisha binti yake huyu anakua katika maadili yaliyo bora na nidhamu yake iwe ya hali ya juu. So nini haswa kilitokea mpaka akawa si mtoto mzuri yule ambaye Mama alifanya kila aliwezalo kuhakikisha anakua hivyo miaka ya nyuma? Sasa ni Mama na mfanyabiashara anayejielewa tu. Ila yepi haswa ambayo yalishawahi kutokea kwenye maisha yake na ambayo hajivunii hata kidogo?


    Mimi na K tunafahamiana miaka mingi sana, mara ya kwanza tulikuna kwenye michezo, kwenye uwanja wa basketball wa Pazi pale Drive In enzi hizo, skuizi nadhani panaitwa Ubalozi maana ni mkabala kabisa na ubalozi wa Marekani na uwanja umo ndani ya nyumba za Tanesco na sisi pia tulikua tukipaita hivyo. I remember alikua anakuja kucheza na sisi enzi hizo yeye anasoma Jitegemee nami nasoma Makongo Secondary School, hakua mchezaji mkaaali ila alikua na juhudi, na kwa mujibu wa maongezi yetu haya aliniambia ile pia ilikua ni moja ya njia zake za kutoka nyumbani na kupata kijihewa ivi, kwa kukutana na watu tofauti 😀. Sisi tulikua tukimshangaa kwa mitkasi yake mingi, alikua anatoka, yuko na marafiki ambao walikua wakubwa kuliko yeye na kama alikua na mambo mengi ivi. Ila huko ndo kukua sasa, maana unachojifunza wakati unafanya jambo ndo hapo unapoweza kujua kama ni zuri au baya na kama lina faida nawe au laa.

    Next thing I know Kajala ni mpenzi wa producer mataaata haswa enzi hizo ndani ya P-Funk na kwenye story zetu za humu amezungumzia hilo kwa urefu haswa, vile walivyokutana, alivyokua anakaa nae, reaction ya wazazi wake na waalimu shuleni na mahusioano yao mpaka yalipofika tamati. Jinsi ambavyo walikua wakiishi yeye na PFunk bila ya Mama yake Majani kujua kama mwanae anaishi na mwanafunzi ndani ya nyumba yake na mpaka akapata mimba bila ya yeye kujua. Paula alipozaliwa ndo mambo yakawa hadharani.

    Mapenzi yake na PFunk yalikua na mambo mengi ambayo niliyauliza kwenye episode hii ya 35, walikutanaje, waliendeleaje, wazazi, Paula na pengine watu wengine kuhusika na mapenzi yao hayo. Aliniambia mwisho wa siku ilibidi afanye liwezekanalo ili aweze kutoka humo na maisha yaendelee na akafanikiwa kukutana na mtu mwengine Ila na kwake naye mambo hayakua matamu kama ambavyo yalianza. Yaliisha kwa machozi na chuki ambayo anadhani iko upande
    wa pili zaidi maana kwake maisha yamesogea na maombi yake ya kuanza upya yamebarikiwa.

    Kajala amepitia mambo mengi kwenye maisha yake ambayo mengine anajivunia na mengine siyo hata kidogo. Kama kawaida, yangu matumaini utaokota mawili matatu humu na ambayo pia kama nia na madhumuni yatakufanya ushangae na kujifunza mwisho wa siku. Tafadhali enjoy!

    Love,
    Salama.

    57 min
  • Ep. 34 - Salama Na DOGO JANJA | YENTE

    Nakumbuka mara ya kwanza kukutana na Dongo Janja enzi hizo akiwa mtoto kabisa na hata kwenye viduara vyetu alikua anakaa mbali maana havikua vinamhusu. Kukua kwake kwenye macho yetu wakati mwengine inatufanya tuwe tunadhani kama tunamfahamu sana au tuna haki sana ya kujua kila kitu kwenye maisha yake na kumhukumu kwa maamuzi mengine ambayo sisi kama sisi hatujayapenda, tunasahau kama hayo ni maisha yake na ana haki ya kujifunza kwa kukosea na kukaa sawa kama ambavyo yuko sasa.


    Jina la serikali ni Abdulaziz Abubakar Chende aka JANJARO, sio DOGO JANJA tena, sasa ana miaka 25. Unakumbuka mara ya kwanza kumuona au kusikia kuhusu yeye? Basi toka siku hiyo mambo yamebadilika sana sana. Ya ki maendeleo na ya ki binafsi kama binadamu. Kwasababu mimi ni Dada yake ilibidi turudi nyuma kidogo maana sijamuona siku nyingi so nilitaka ku catch up wazungu wanasema. Kwanza nimeona kwa ukaribu kama hana tena ile sura ya ki toto na confidence yako ni ya mtu aliyepitia kadhaa na akajifunza juu yake.

    Khadithi kuhusu siku ya kwanza alipofika hapa jijini Dar es Salaam, alifikaje? Alikuja kufanya nini? Je yeye kujulikana akiwa na umri mdogo anadhani kumemtegenezea maisha yake au kumemzigua? Mahusiano yake na Rais wa Manzese, TIp Top Connection na pia kuhusu elimu ambayo kwa kipaji chake ni kama alikua akiipata kwa bei nafuu tu. Ilikuaje mpaka akashindwa kabisa kumaliza? Miaka si mingi pia alimpoteza Baba yake mzazi ambaye kwa mujibu wa Abdul walikua ni watu wa karibu sana na kifo chake kilimgusa ki vyengine sana.

    Kuna suala la ndoa ambayo wengi wetu tulidhani ilikua kama geresha ivi au Kiki kama wasemavyo watoto wa mjini. Kumbe ilikua na ukweli kabisa na wawili hao walikua wameshibana mpaka wakaona waoane tu. So nini kilitokea hapo mpaka sasa hawako pamoja? Kwanini anadhani ilikua habari kubwa ambayo ilikua Ina nenda rudi nyingi? Je ana majuto yoyote kuhusu suala hili kwa ujumla yeye kama yeye? Na vipi kuhusu maisha yake ya sasa? Ana furaha? Aliye naye anadhani ndo wa kweli kwake? Pia kuna suala la muziki na umaarufu na suala la Mama yake na mahusiano yao kama Mama na mtoto wake.

    Janjaro kakua na nimeliona hilo kwa jinsi tu anavyojibeba na anavyojielewa, hana papara katika kujibu maswali na kutafakari vitu, na kwa asilimia 100 naamini limetokana na kukaa na Madee karibu kwasababu nimeambiwa katika watu wenye busara na maamuzi ya kuto kukurupuka kwenye vitu basi Rais wa Manzese naye yumo. Napenda kumpogeza kwa kukuza na kuendelea kumsuka kijana awe kati ya binadamu bora. Nakutakia utazamaji mwema kwenye kipindi hiki na yangu matumaini utajifunza jambo na uta enjoy pia.

    Love,
    Salama.

    49 min

About Salama Na

From the publisher's feed

‘Salama na’ – meaning ‘Salama and’ is a one hour Podcast chat show hosted by a re known Radio &; TV personality Salama Jabir and available on Both Video and Audio of Various Platforms. In Salama…