Mkurugenzi wa Idara ya Baishara katika Benki ya Absa, Susan Situma amesema ili uchumi wa taifa uimarike, ni sharti wanawake wajumuishwe. Amekariri kwamba kuna haja ya serikali kuwashirikisha wajasiriamali wanawake ili pato la taifa likue.
Kwa mujibu wa Situma, Benki ya Absa imezindua akaunti ya Absa She Account inayolenga kuhakikisha wafanyabiashara wadogo wadogo hususan wanawake wanapata fursa ya kuwekeza na kuomba mikopo hadi shilingi milioni kumi.
Aidha, amewasihi wanawake na Wakenya kwa jumla kuchukua bima ya maisha ili kusaidika wanaposhindwa kulipia mikopo ya benki. Amesema wakati huu wa korona, wateja wengi wa Absa waliokuwa wamechukua mikopo walilipiwa na bima mbalimbali hasa baada ya biashara zao kuathirika.
Situma amezungumza na mwanahabari wetu Esther Kirong' na anasema kando na Absa kuwawezesha wafanyabiasha, vilevile inawapa ushauri nasaha jinsi watakavyotumia fedha za mikopo vilevile kuwekeza.