Tunaangazia hali ya Ziwa Victoria, changamoto zinazolikabili pamoja na juhudi za kikanda zinazofanyika kulinusuru ziwa hilo ambalo ni mhimili wa uchumi na maisha ya wananchi wa Afrika Mashariki.
Ziwa Victoria, ambalo ni tegemeo la mamilioni ya wananchi wa Afrika Mashariki, linaendelea kukumbwa na changamoto kubwa za mazingira, uvuvi haramu na uchafuzi wa maji.
Ripoti mpya ya mwaka 2025 imeonya kuwa bila hatua za haraka, uchumi, afya na maisha ya wananchi wa ukanda huo yako hatarini.
Jumuiya ya Afrika Mashariki imezindua ripoti ya mwaka 2025 kuhusu hali ya Bonde la Ziwa Victoria, ikieleza changamoto zinazoendelea kulikabili ziwa hilo ikiwemo uvuvi haramu, uchafuzi wa mazingira na kupungua kwa samaki muhimu wa biashara.
Ripoti hiyo yenye sura tisa imechambua kwa kina hali ya ikolojia, mazingira, viwanda, mipango miji, ajira, utalii pamoja na maendeleo ya miundombinu katika ukanda wa Ziwa Victoria.