Habari za UN - Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Habari za UN - Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

By United NationsNewsDaily News
Download on the App Store

Habari za UN - Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu episodes

  • UNHCR Sudan Kusini yachukua hatua kupunguza madhara ya mafuriko katika sekta ya kilimo
    Huko Maban, jimboni Upper Nile, kaskazini mashariki mwa Sudan Kusini, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi ,UNHCR linajenga vifaa vya kuhifadhi maji pamoja na makinga maji ili kuepusha mashamba dhidi ya mafuriko ya msimu yanayokumba eneo hilo mara kwa mara, eneo ambalo ardhi yake ina rutuba kwa ajili ya kilimo cha mazao ya chakula na biashara. Hapa shambani jimboni Upper Nile nchini Sudan Kusini, wakulima wakiwemo wenyeji na wakimbizi wakiwa shambani wakiimba.  Awad Usman mwenyeji wa hapa anasema kuimba kunatuliza fikra zangu. Nyimbo hazisaidii kupanda mazao, lakini zinaweza kupunguza msongo wa mawazo.Msongo wa mawazo unatokana na madhara ya mabadiliko ya tabianchi yaletayo mvua kubwa na mafuriko kwenye mashamba yao.Awad anasema nakumbuka mafuriko ya mwaka 2019, yalisomba kila kitu. Ufuta wote ulisombwa. Mtama pekee ulisalia. Tulikaa ndani ya nyumba kwa siku tano, na tulipotoka tulikuta shamba zima limetwama kwenye maji.Alex Noel Kilong, afisa wa UNHCR anasema mafuriko yanaongeza machungu kwa shida ambazo tayari jamii inakumbana nazo. Mafuriko yanazidi kuongezeka na kusoma barabara, mifugo, mashamba na vituo vya afya hivyo anasema..“Tunahitaji kujenga mbinu za kujipatia kipato. Maban ina fursa kubwa sana, udongo una rutuba, tunatakiwa pia kujenga mapipa ya kuhifadhi maji juu ya ardhi, na maji haya yanaweza kutumiwa wakati wa ukame, ili kilimo kiwe shughuli inayoweza kufanyika mwaka mzima. Kwa njia hiyo tutaweza kupunguza njaa. Tutapunguza ukosefu wa uhakika wa chakula miongoni mwa wenyeji na pia kwa wakimbizi.UNHCR pia imepatia wakulima kama Awad mbegu ya ufuta mweupe, ambayo anasema ni bora na hivyo atakavyovuna , kiasi atauza na nyingine atahifadhi kwa matumizi ya kula nyumbani na pia kama mbegu.
    3 min
  • 12 NOVEMBA 2024
    Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina inayotupeleka Havana Cuba amabpo Flora Nducha amaezungumza na mshiriki kutoka maitaifa mbalimbali na leo ni Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo DRC. Pia tunakuletea muhtasari wa habari na mashinani inayotupeleka Zimbabwe.Kuongeza kiwango cha fedha kwenye ufadhili wa miradi ya kukabili na kuhimili tabianchi nchi ikiwa ni moja ya masuala muhimu yanayojadiliwa katika mkutano wa 29 wa nchi wanachama wa mkataba wa mabadiliko ya tabianchi, COP29 huko Baku, Azerbaijan, leo ikiwa ni siku ya pili ya mkutano huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema bila kupunguza kwa kiasi kikubwa hewa chafuzi, na kuimarisha miradi ya kuhimili na kukabili mabadiliko ya tabianchi, kila uchumi duniani utakumbwa na madhara makubwa.Ripoti mpya ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR iliyotolewa leo huko COP29 inaonesha ni kwa jinsi gani watu wanaokimbia vita, ghasia na mateso wanazidi kujikuta kwenye mazingira yaliyokumbwa na janga la tabianchi, janga ambalo linawaweka kwenye mchanganyiko wa vitisho, lakini bila fedha wala msaada wa kukabiliana navyo.Na mamia ya wakimbizi wanaotaka kujiunga na elimu ya juu sasa watafanya bure mitihani ya kuonesha umahiri wao wa lugha ya kiingereza, au IELTS. Hii inafuatia makubaliano ya ushirikiano kati ya UNHCR na mfumo wa kimataifa wa lugha ya kiingereza, IELTS.Na mashinani COP29 ukiendelea huko Baku Azerbaijan, tunabisha hodi  nchini Zimbabwe ambako Umoja wa Mataifa unawasaidia wakulima kakabiliana na mabadiliko ya tabianchi.Mwenyeji wako ni Assumpta Massoi, karibu! 
    10 min
  • Kozi za Kiswahili ziongezwe ili watu wengi zaidi wajifunze duniani kote- 'Bongo Zozo'
    Kongamano la kimataifa la Kiswahili limefunga pazia mwishoni mwa wiki mjini Havana Cuba ambako washiriki takriban 400 kutoka barani Afrika, Ulaya, Asia na Aamerika wamejadiliana mada mbalimbali za kukuza na kupanua wigo wa lugha hiyo ya Kiswahili duniani. Hata hivyo wapenzi wa lujifunza lugha hiyo wanataka kozi za kujifunza Kiswahili kwa wageni ziongezwe katika sehemu nyingi zaidi ili kutoa fursa kubwa kwa wanaotaka kujifunza kama alivyobaini Flora Nducha alipozungumza na mmoja wa wachechemuzi wa lugha hiyo ya Kiswahili Nick Reynold au Bongo Zozo. Ungana nao katika Makala hii
    4 min
  • Stiell: Lazima tuweke malengo ya juu ya ufadhili ili kukabili mabadiliko ya tabianchi
    Kufuatia mwaka mwingine wa viwango vya juu vya joto kali na matukio ya kupitiliza ya hali ya hewa, Mkuu wa Sekretarieti ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Tabianchi Simon Stiell amewaeleza washiriki wa mkutano wa 29 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi, COP29 , kwamba malengo mapya ya ufadhili kwa tabianchi ni muhimu kwa ajili ya ustawi wa mataifa, yakiwemo yale tajiri na yenye uthabiti. Katika hotuba yake mbele ya washiriki wa mkutano huo ulioanza leo huko Baku, mji mkuu wa Azerbaijan hadi tarehe 22 mwezi huu wa Novemba, Bwana Stiell amesema kwa kadri madhara ya mabadiliko ya tabianchi yalivyo dhahiri ni lazima kukubaliana mwelekeo mpya wa ufadhili kwa miradi ya kukabili na kuhimili.Amehoji, mnataka bei za vyakula na nishati iongezeke zaidi? Je mnataka nchi zenu ziendele kushindwa kushindana kiuchumi? Je mnataka dunia yetu iendelee kukosa utulivu na kugharimu maisha adhimu?Amekumbusha kuwa janga la tabianchi linaathiri kila mkazi wa dunia kwa njia moja au nyingine.Bwana Stiell amesema nimekanganyikiwa kama mtu mwigine yeyote kwamba mkutano mmoja wa COP hauwezi kuleta marekebisho abayo kila taifa linahitaki. Lakini iwapo majibu yenu kwenye maswali hayo ni HAPANA, basi ni hapa pande zote zinahitaji kukubaliana jinsi ya kuondokana na zahma hii.Hivyo amesema, “katika nyakati ngumu, kukiwa na majukumu mazito, sitegemei matumaini na ndoto. Kinachonihamasisha ni stadi na azma ya binadamu. Uwezo wetu wa kuanguka na kuinuka tena na tena, hadi tunapotimiza malengo yetu.”Amekumbusha kuwa mkataba wa tabianchi ndio mchakato pekee ambapo wanaweza kupatia majawabu janga la tabianchi na kuwajibishana kwa wale wanaokwenda kinyume.Ametaka washirika kuonesha stadi zao kwenye COP29 na pande zote zishinikize makubaliano ya ufadhili kwa tabianchi la sivyo kila nchi itagharimika.
    3 min
  • 11 NOVEMBA 2024
    Hii leo jaridani tunaangaziamkutano wa 29 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi, COP29, na mradi wa lishe bora kwa watotot Afar nchini Ethiopia. Makala inatupeleka Havana Cuba na mashinani tunasalia huko huko Havana Cuba, kulikoni?Kufuatia mwaka mwingine wa viwango vya juu vya joto kali na matukio ya kupitiliza ya hali ya hewa, Mkuu wa Sekretarieti ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Tabianchi Simon Stiell amewaeleza washiriki wa mkutano wa 29 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi, COP29, kwamba malengo mapya ya ufadhili kwa tabianchi ni muhimu kwa ajili ya ustawi wa mataifa, yakiwemo yale tajiri na yenye uthabiti.Mradi wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF wa kuchagiza kaya kulima bustani za mboga za majani pamoja na ufugaji wa kuku huko jimbo la Afar, kaskazini mashariki mwa Ethiopia umesaidia familia za vijijini kukabiliana na utapiamlo miongoni mwa watoto.Makala inatupeleka Havana Cuba ambako kongamano la kimataifa ka Kiswahilii limekunja jamvi mwishoni mwa wiki na shuhuda wetu huo Flora Nducha amezungumza na watu mbalimbali akiwemo mchechemuzi wa Kiswahili hususan kwenye mitandaao ya kijamii Nick Reynold ali maarufu Bongo Zozo, ambaye ni raia wa Uingereza.Na mashinani fursa ni yake Profesa msaidizi Xiaoxi Zhang raia wa China ambaye ni mshirika wa kimataifa au (Global Fellow) na mhadhiri wa masuala ya fasihi linganishi katika chuo kikuu cha Habib kilichopo Sindhi Karachi nchini Pakistan mmoja wa waliohudhuria kongamano la Kiswahili lililomalizika mwishoni mwa wiki akitoa ujumbe kuhusu changamoto ya kujifunza  Kiswhili.Mwenyeji wako ni Bosco Cosmas, karibu! 
    10 min
  • Mradi wa UNICEF wa kuboresha lishe waleta tabasamu kwa wazazi na watoto Afar Ethiopia
    Mradi wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF wa kuchagiza kaya kulima bustani za mboga za majani pamoja na ufugaji wa kuku huko jimbo la Afar, kaskazini mashariki mwa Ethiopia umesaidia familia za vijijini kukabiliana na utapiamlo miongoni mwa watoto. Video ya UNICEF Ethiopia inaanza ikimuonesha mtoto akitabasamu, na kisha akiwa na mama yake wakielekea kwenye kituo cha afya. Mama huyu anaitwa Fatuma Kebir na mwanae huyu aliyembeba anaitwa Abdu. Fatuma anasema..“Nilihofia kuwa angeendelea kuwa na utapiamlo. Kwa hiyo nilimpeleka kituo cha afya na mhudumu wa afya akanieleza kuwa mwanangu amepoteza uzito, kama ambavyo nilihisi. Akaniambia nimlishe zaidi, hasa uji uliochanganywa na mayai, maziwa, na mboga.”Video ikimuonesha Fatuma akiandaa uji akichanganya na mayai, mtaalam wa lishe wa UNICEF, Yetayesh Maru, anasema,“Kama sehemu ya mtambuka wa hatua na uratibu dhidi ya utapiamlo kwenye jamii, Fatuma ametambuliwa kuwa ni kaya iliyo hatarini, hivyo amenufaika na mradi wa kisekta wa kuboresha lishe kwa watoto.”Sasa Fatuma na mtoto wake Abdu wanapata tabasamu upya.“Nilimlisha kwa mwezi mmoja kama walivyoshauri na kisha nikarudi kituo cha afya. Mtoa huduma alisema kwamba sasa ana afya na amerudia uzito wake. Nilifurahi sana alipoanza kuongezeka uzito.”Tabasamu lao ni dhahiri hata kwa mtoa huduma Yetayesh, akisema “Sasa Abdul anakua vizuri, na nguvu kamilifu, huku akicheka na mama yake.”
    2 min
  • Tutahakikisha Kiswahili kinasambaa duniani na kusongesha ajenda za UN: Dkt. Ndumbaro
    Kongamano la kimataifa la Kiswahili leo limeng’oa nanga jijini Havana Cuba likiwaleta pamoja takribani washiriki 400 kutoka Afrika, Asia, Amerika na Ulaya ili kujadili ajenda mbalimbali za kupanua wigo wa luugha hiyo na kuitumia kuleta tija ikiwemo kusongesha malengo ya Umoja wa Mataifa kama amani na maendeleo endelevu. Akizungumza na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa wakati wa Kongamano hilo Waziri wa utamaduni, sanaa na michezo wa Tanzania Dkt. Damas Daniel Ndumbaro amesema hili ni kongamano la kimataifa la Kiswahili na ajenda yake kuu ni kukifanya Kiswahili kivuke mipaka. 
    6 min
  • 08 NOVEMBA 2024
    Hii leo jaridani tunakuletea kipindi maalum kinachotupeleka jijini Havana Cubaambapo kongamano la kimataifa la Kiswahili limeng’oa nanga likiwaleta pamoja takribani washiriki 400 kutoka Afrika, Asia, Amerika na Ulaya ili kujadili ajenda mbalimbali za kupanua wigo wa luugha hiyo na kuitumia kuleta tija ikiwemo kusongesha malengo ya Umoja wa Mataifa kama amani na maendeleo endelevu.Miongoni mwa habari kubwa Umoja wa Mataifa hii leo ni uwajibikaji unasakwa kwa ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu dhidi ya  wapalestina na waisraeli, na pia shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo, FAO limeweka bayana gharama za kiuchumi na hata kiafya zilizofichika zitokanazo na mifumo ya uzalishaji, usafirishaji na ulaji wa chakula. Lakini kubwa zaidi nakupeleka Havana, Cuba kupata kwa mahtasari mazungumzo ya Flora Nducha na mmoja wa washiriki.Mashinani tunasalia huko huko Havana Cuba na fursa ni yake Profesa Juan (Huani) Jacomino (Hakumino) raia wa Cuba ambaye ni Mwalimu wa Kiswahii katia  chuo kikuu cha Havana Cuba anayeshiriki Kongamano la Kiswahili lililofunguliwa leo akitoa wito kwa raia wa Cuba na wa nchi zingine kuhusu umuhimu wa kukumbatia  Kiswahili. Mwenyeji wako ni Bosco Cosmas, karibu! 
    10 min
  • 07 NOVEMBA 2024
    Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina inayotupeleka huko Havana Cuba kwenye Kongamano la kimataifa la Kiswahili kusikia kutoka kwa waziziri Zanzibar kuhusu faida za kiplomasia na kiuchumi. Pia tunakuletea muhtasari wa habari na ujumbe kuhusu Kiswahili.Fedha kwa ajili ya mipango ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, ni jambo lililopatiwa kipaumbele katika ripoti mpya ya leo ya shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira, UNEP wakati huu ambapo kiwango cha joto kinazidi kuongezeka kila uchao na kuleta zahma duniani kote.Shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO linasema hii leo watoto 6 wa kipalestina, wamesafirishwa kutoka Gaza kwenye Romania kwa matibabu mahsusi ; watatu wakiwa wanaugua saratani, wawili magonjwa ya  damu na mmoja majeraha. Wameambatana na jumla ya waangalizi 15.Na huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo, MONUSCO umezindua mfumo wa uthibitishaji, kama sehemu ya mchakato wa Luanda wenye lengo la kufuatilia makubaliano ya sitisho la mapigano kati ya Rwanda na DRC yaliyoanza kutekelezwa tarehe 4 mwezi Agosti mwaka huu mashariki mwa taifa hilo la Maziwa Makuu.Katika kujifunza lugha ya Kiswahili tunasalia huko huko Havana Cuba, kwenye kongamano la Kiswahili la Kimataifa ambako Dkt. Kisembo Ronex Tendo mshiriki kutoka taasisi ya vijana ya Afrika Mashriki Fest Uganda anaeleza cha kufanya kusongesha Kiswahili nchini Uganda.Mwenyeji wako ni Assumpta Massoi, karibu! 
    12 min

About Habari za UN - Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

From the publisher's feed

Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

More shows like Habari za UN - Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ONU Info - L'actualité mondiale Un regard humain by United Nations

ONU Info - L'actualité mondiale Un regard humain

14 Listeners

ONU en minutos by United Nations

ONU en minutos

43 Listeners

ONU News - Perspectiva Global Reportagens Humanas by United Nations

ONU News - Perspectiva Global Reportagens Humanas

5 Listeners

UN News Today by United Nations

UN News Today

95 Listeners

联合国新闻 - 全球视野, 常人故事 by United Nations

联合国新闻 - 全球视野, 常人故事

25 Listeners

Новости ООН - Глобальный взгляд Человеческие судьбы by United Nations

Новости ООН - Глобальный взгляд Человеческие судьбы

9 Listeners

أخبار الأمم المتحدة - منظور عالمي قصص إنسانية by United Nations

أخبار الأمم المتحدة - منظور عالمي قصص إنسانية

18 Listeners

यूएन समाचार - वैश्विक परिप्रेक्ष्य मानव कहानियां by United Nations

यूएन समाचार - वैश्विक परिप्रेक्ष्य मानव कहानियां

4 Listeners

UN Interviews by United Nations

UN Interviews

6 Listeners

UNcomplicated by United Nations

UNcomplicated

15 Listeners

The Lid is On by United Nations

The Lid is On

8 Listeners

UN Weekly by United Nations

UN Weekly

9 Listeners

UNiting Against Hate by United Nations

UNiting Against Hate

4 Listeners

amplifyHER by United Nations

amplifyHER

4 Listeners

世界进行时 by United Nations

世界进行时

0 Listeners

前方视野 by United Nations

前方视野

0 Listeners

Podcast ONU News by United Nations

Podcast ONU News

0 Listeners

Actualités by United Nations

Actualités

0 Listeners