Tuliyokuandalia ni pamoja na bodi mpya ya uchaguzi wa shirikisho la soka nchini DRC, waziri wa michezo nchini Tanzania Damas Ndumbaro abainisha viwanja 20 kwa ajili ya AFCON 2027, timu ya REG nchini Rwanda yafuzu Ligi ya Basketboli Afrika 2024 kwa kina dada, mechi za kufuzu CHAN 2025, hatma ya kocha wa Rwanda Torsten Spittler, Senegal kuandaa michezo ya Olimpiki ya kwanza barani Afrika ya chipukizi mwaka 2026, kocha mpya wa Man Utd, mashindano ya Paris Masters na Brazilian GP
Afrika inatarajia michezo ya kwanza ya Olimpiki ya vijana itakayoandaliwa barani Afrika mwaka 2026, jijini Dakar, mji mkuu wa Senegal.
Michezo hiyo imepangwa kufanyika kati ya Oktoba 31 na Novemba 13, 2026, tukio ambalo litaleta pamoja wanariadha bora zaidi ulimwenguni kushiriki katika michezo 35 tofauti kwa siku 14.
Tamasha la Dakar en Jeux (Dakar in Games) lilipangwa awali kwa kipindi cha Dakar 2022, katika miji mitatu ya mwenyeji wa Dakar, Diamniadio, na Saly.
Tangu wakati huo, Dakar en Jeux imekuwa sherehe ya kila mwaka ya michezo na utamaduni, ikihudumu kama mtangulizi wa Dakar 2026 wakati ikihimiza kuongezeka kwa ushiriki wa vijana katika michezo.
Rais wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC) Thomas Bach ameripotiwa kuunga mkono Senegal kuandaa Michezo ya Olimpiki ya Vijana, akibainisha umoja wa Afrika na utamaduni wake wa michezo.
"Kwa idadi ya vijana na shauku ya michezo, ni wakati wa Afrika, ni wakati wa Senegal," alisema katika ripoti ya olympics.com.
"Hatuwezi kusubiri muda urudi hapa na kufurahia tukio hili la kwanza la Olimpiki katika ardhi ya Afrika, ambalo litawakaribisha vijana wa dunia nchini Senegal." Bach alitoa matamshi hayo wakati wa ziara yake nchini Senegal mwaka 2022, akifichua matarajio yake ya tukio hilo.
Wachambuzi wa michezo kutoka sehemu mbalimbali za Afrika wanachukulia tukio hilo kuwa la kihistoria huku Rufai Shuaib kutoka Senegal akisema;
"Kuandaa Michezo ya Olimpiki ya Vijana huko Dakar inawakilisha hatua kubwa katika kuonyesha talanta kubwa na uwezo wa wanariadha wetu wachanga kwenye jukwaa la kimataifa," alisema.
Taarifa ya ziada: Olympics