Kila mwaka inapofika wakati wa kusherehekea sikukuu ya Pasaka, yaani kufufuka kwake Yesu Kristo msalabani, kumbuka suala moja la msingi sana- kushindwa kwa mauti. Kutokana na Yesu kufufuka katika wafu mauti imeshindwa milele kwa sababu Yesu anaishi milele. Na ndio maana mahali pengine ameitwa mzaliwa wa kwanza wa waliokufa, siyo kwa sababu yeye ndio wa kwanza kufufuka- manabii Elia na Elisha walitumiwa kufufua wafu pia, yeye ndio wa kwanza kufufuka katika wafu na kuishi milele. Hii ni alama kwetu kwamba wote waliolala katika imani watafufuliwa na kuishi milele pamoja nae. Kama yeye mwenyewe alivyosema mtu akimuamini hata akifa bado anaishi. Mauti imeshindwa, kwa hiyo usiogope mauti kwa sababu haina kitu kwako. Biblia inasema usiogope.